Beki wa kulia wa ‘Wekundu wa Msimbazi’ Simba Hassan Kessy ametimka kikosini na kuelekea nyumbani kwao Morogoro baada ya uongozi wa klabu hiyo ya Msimbazi kushindwa kumtafutia nyumba ya kuishi.
Kessy amesema kuwa, katika makubaliano yake na Simba walimuahidi wangempa nyumba ya kuishi lakini hali imekua tofauti kwani amekua akiishi kama ‘njiwa’ na uongozi hauonekani kujali. Amesema mbaya zaidi ni pale wachezaji wengine wanapoonekana ni muhimu kwenye klabu na kujaliwa kuliko wengine.
“Simba waliniahidi wangenitafutia nyumba, lakini toka nimekuja Dar es Salaam nimekuwa nikikaa kwa watu tu, mara leo hapa kesho pale. Nataka niwe na sehemu ya kupumzika, nikitoka kazini narudi nymbani kwangu, lakini Simba wameshindwa kutekeleza hilo, amesema Kessy.
“Nimeamua kurudi nyumbani Morogoro hadi hapo mambo yatakapokuwa sawa, nikihakikishiwa nyumba na pesa yangu nayodai nitarejea kuendelea na kazi. Mpira ni kazi yangu, sasa kama watu wanakuwa hawajali kazi yangu siwezi kuwaelewa,” ameongeza Kessy.
Meneja wa mchezaji huyo Athumani Tipo amesema, Simba walikubali kumtafutia Kessy nyumba ya kuishi lakini imekuwa tofauti, na kila anapowatafuta viongozi wa timu ili kutaka kujua hatma ya mchezaji huyo wamekuwa hawapokei simu yake.
“Simba walikubali kumtafutia Kessy nyumba ya kuishi lakini toka amejiunga na kikosi hicho mambo yamekuwa tofauti, amekuwa anaishi kwa watu hadi ameamua kurudi nyumbani mpaka hapo tutakapoweka mambo sawa. Lakini pindi napowatafuta viongozi wa Simba ili kujua tutalitatua vipi suala hili wamekuwa hawapokei simu zangu na kuleta ‘ujanjaujanja’” amesema Tipo.
Afisa habari wa Simba Haji Manara yeye amesema mchezaji huyo hayupo kwenye kikosi kutokana na matatizo ya kifamilia, lakini alipobanwa zaidi akasema hakuna mtu anayejua mkataba wa Kessy na Simba ukoje hivyo inawezekana malalamiko ya Kessy yakawa hayapo kwenye mkataba.
Leo kikosi cha Simba kimesafiri kuelekea Shinyanga kwa ajili ya mchezo wake dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa Jumamosi kwenye uwanja wa CCM Kambarage lakini Kessy hayupo kwenye kikosi kilichosafiri leo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni