Louis
van Gaal ameeleza kuwa uamuzi wa kumuingiza Kipa wa Akiba Tim Krul kwa
ajili ya Mikwaju Mitano Mitano ya Penati walipocheza Robo Fainali ya
Kombe la Dunia na Costa Rica ulikuwa umepangwa.
Netherlands wametinga Nusu Fainali kutokana na ushujaa wa Kipa Krul ambae aliokoa Penati mbili.
Kipa Tim Krul aliingizwa kumbadili Kipa
Nambari Wani Jasper Cillessen zikiwa zimebaki Sekunde 44 kabla ya
Filimbi ya mwisho ya Dakika 120 za Mchezo na kuokoa Penati mbili wakati
Netherlands ikiibwaga Costa Rica kwa Mikwaju ya Penati 4-3 baada Timu
hizo kwenda 0-0 kwa Dakika 90 na Nyongeza ya Dakika 30 kubaki hivyo
hivyo.
Van Gaal, ambae ataanza kazi huko
Manchester United mara baada Fainali za Kombe la Dunia kwisha, ameeleza:
“Tulimwambia Krul kwamba upo uwezekano wa Penati lakini hatukumwambia
Jasper Cillessen kama tutambadili kwa Penati. Hatukutaka kuharibu
matayarisho yake!”
Van Gaal aliongeza: “Hamna utata nani ataanza Mechi ijayo, atakuwa ni Cillessen. Kwa Penati, tulihisi Krul ni bora!”
Alieleza: “Tunajua Krul ni mzuri kwa
Penati, ni mrefu pia. Tulifanyia Mazoezi Penati na nadhani ukizoea aina
fulani ya shuti unakuwa mtulivu kwa shuti la aina hiyo hiyo.”
Kuhusu Kikosi chake, Van Gaal alisema:
“Hiki ni Kikosi bora ambacho nimewahi kufanya nacho kazi. Hasa kwa ari
ya kitimu na umoja.”
Netherlands itakutana na Argentina
kwenye Nusu Fainali Jumatano ijayo huko Sao Paulo ikiwa ni kama marudio
ya Fainali ya Kombe la Dunia ya Mwaka 1978 huko Buenos Aires, Argentina
ambayo Wenyeji walishinda 3-1 katika Dakika za Nyongeza 30.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni