AZAM FC waliibuka mabingwa wa ligi kuu soka
Tanzania bara msimu uliopita kwa kuwashinda waliokuwa washindani wao wakubwa,
Yanga sc na Mbeya City fc kwa mbali.
Hizi ni rekodi za mabao msimu wa 2013/2014 ambao
ulikuwa na ushindani mkubwa hususani katika mbio za ubingwa.
Azam fc ndio timu iliyofungwa mabao machache zaidi
kuliko timu zote 14 za ligi kuu ambapo iliruhusu nyavu zake kuguswa mara 15 tu.
Yanga sc ndio timu iliyofunga mabao mengi zaidi
msimu uliopita ambao ilitikisha nyavu za wapinzani mara 61.
Azam ilikuwa timu ya pili kufunga mabao mengi
ambapo ilitia kambani magoli 51.
Licha ya Yanga kufunga mabao mengi, lakini
ilifungwa magoli mengi ukilinganisha na mabingwa Azam ambapo iliruhusu nyavu
zake kuguswa mara 19 .
Mbeya City na Kagera Sugar zilikuwa timu
zinazofuatia kufungwa mabao machache zaidi ambapo kila moja iliruhusu nyavu
zake kuguswa mara 20.
JKT Ruvu ndio timu iliyofungwa mabao mengi zaidi
msimu uliopita ambapo nyavu zake ziliguswa mara 40, ikifuatiwa na timu za Rhino
Rangers na Ashanti United zilizofungwa mabao 39.
Rhino na Ashanti zilishashuka daraja na kuzipisha Stand
United ya Shinyanga, Ndanda fc ya Mtwara na Polisi Morogoro ya mkoani Morogoro.
Kwa kuangalia takwimu hizi za mabao unaweza
kusema:
Azam fc ndio timu iliyokuwa na safu bora zaidi ya
Ulinzi ikifuatiwa na Dar Young Africans.
Aggrey Morris, Said Mourad Mwenda, David Mwantika,
Erasto Nyoni, Gadile Michael na wengineo, walifanya kazi nzuri zaidi ya mabeki
wa timu zote 14 za ligi kuu.
Kwa upande wa Yanga, Nadir Haroub `Canavaro’,
Kevin Yondan, Oscar Joshua, Mbuyu Twite na wengineo walijitahidi kufuata nyayo
za mabeki wa Azam fc.
Mbeya City na Kagera zilishika nafasi ya tatu kuwa
na safu imara ya ulinzi kwa maana ya kuruhusu magoli machache.
Yanga ndio timu iliyokuwa na safu kali zaidi ya
ushambuliaji ikifuatiwa na Azam fc, lakini moja ya mshambuliaji wake, Didier
Kavumbagu ameshaondoka.
Lakini wamewasajili Wambrazil wawili, kiungo
mshambuliaji, Andrey Coutinho na mshambuliaji Gleison Santos Santana ‘Jaja’.
Pengi wataziba pengo hilo, ingawa wanatakiwa kumuacha mchezaji mmoja wa kigeni
baada ya kuzidisha idadi.
Niyonzima, Twite, Kiiza na Okwi, lazima mmoja
nyumba imuangukie. Lakini inaonakana vita ni kati Okwi na Kiiza, lazima mmoja
aondoke.
JKT Ruvu ndio timu iliyokuwa na safu mbovu zaidi
ya ulinzi kuliko timu zote 14. Kwa maana hiyo, safu ya ulinzi lazima iimarishwe
wakati huu wa usajili pamoja na kutafuta viungo watakaotoa msaada kwa mabeki.
Kwa kuzingatia takwimu hizi za mabao, inategemewa
kuona Azam fc inaongeza nguvu safu ya kiungo na ushambuliaji. Kwa maana ya
kupata viungo watakaochezesha safu yao ya ushambuliaji.
Yanga wanatakiwa kuimarisha kiungo na ulinzi.
Inaonekana licha ya kuwa na washambuliaji wakali, lakini sehemu ya kiungo
iliyumba na kuwapa kazi mabeki kuzuia hatari na matokeo yake kushika nafasi ya
pili kwa kufungwa mabao machache.
Lakini takwimu sio mbaya sana, Yanga ilikuwa timu
ya pili iliyoonekana kuwa imara idara zote, japokuwa kulikuwa na mapungufu
katikati na beki.
Je, wachezaji wanosajiliwa Yanga na Azam ni wa aina gani?
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni