STAY WITH US

LightBlog

Breaking

TANGAZA NASI: +255 655 442 255

TANGAZA NASI: +255 655 442 255

CHANZI OPEN SCHOOL

CHANZI OPEN SCHOOL

Jumatatu, 7 Julai 2014

UWANJA WA YANGA SC BADO NI NDOTO ZA ALINACHA



Uwanja wa Kaunda wakati wa mvua huwa hivi

SERIKALI imesema tathmini ya kina inapaswa kufanywa kabla ya kuiruhusu Yanga kujenga uwanja Jangwani kwa kuwa eneo hilo ni njia kuu ya maji jijini Dar es Salaam.
Desemba 2012 uongozi wa Yanga ulitangaza rasmi kuwa utajenga uwanja wenye uwezo wa kuketisha watazamaji 40,000 kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga Dar es Salaam.
Clement Sanga, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, anasema klabu hiyo ipo katika mikakati ya kujenga Uwanja wake wa Kaunda ili uwe wa kisasa na walipanga kuanza ujenzi huo Juni mwaka jana ukiwa na gharama ya dola za Marekani milioni 21 (Sh. bilioni 32).
Anasema ujenzi huo utafanyika chini ya usimamizi wa Kampumi ya Beijing Constructinon Engineering ya China iliyojenga pia Uwanja wa Taifa na pia kuukarabati Uwanja wa Uhuru jijini hapa.
“Ramani ya Uwanja ambayo tumepatiwa na Wachina inaingia sehemu ya nje ya Uwanja wetu wa Kaunda ambayo ni eneo la wazi la Serikali. Tangu mwaka jana tumeandika barua kwa Manispaa ya Ilala na wizara yenye dhamana ya ardhi kuomba kibali cha ujenzi na kuongezwa eneo la ziada, lakini bado hatujajibiwa, ndiyo maana tumesimama kusubiri majibu ya Serikali,” anasema Sanga.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Uwanja huo, Francis Kifukwe anasema uongozi wa klabu hiyo uliandika barua mara mbili zenye kumbukumbu namba YAC/Ardhi/MWA/46/2012 na YAC/Ardhi/MWA/ 47/ 2012 na mpaka sasa anadai hawajajibiwa.
Awali, Uwanja wa Kaunda pamoja na hosteli ya klabu hiyo vilijengwa mwaka 1973 kwa gharama ya Sh. Milioni 3, sehemu ya fedha hizo zikitoka kwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeif Amaan Karume (sasa marehemu) na nyingine wanachama wakijichangisha.
Hata hivyo, kwa sasa Kaunda hautumiki baada ya kuharibiwa na mafuriko huku ukuta wake ukibomoka kufuatia mvua kubwa iliyonyesha jijini hapa mwanzoni mwa mwaka juzi na Aprili mwaka huu.
Baada ya kupewa kibali cha ujenzi na Serikali, Sanga anasema uongozi wa Yanga unatarajia kusaka benki ambayo itaikopesha klabu hiyo kongwe nchini fedha kwa ajili ya mradi huo. 
Sanga pia anasema uongozi utawaomba wanachama wao 210,000 kuchangia Sh. 250 kwa wiki ili kwa mwaka zipatikane Sh. bilioni nane kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa Uwanja huo.
Hata hivyo, akizungumza katika mahojiano maalum na BIN ZUBEIRY kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini hapa wiki iliyopita, Ofisa mazingira wa ofisi hiyo alisema Serikali haitakuwa na papara kutoa kibali cha ujenzi wa Uwanja wa Jangwani kwa vile eneo hilo ni njia kuu ya maji.
Baada ya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya tathmini ya mradi huo, Ofisa huyo anasema Kurugenzi ya Mazingira ya Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itashauriana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kabla kutoa uamuzi.
“Eneo la Jangwani ni njia kuu ya maji katika jiji la Dar es Salaam, kumekuwa kukitokea mafuriko kutokana na baadhi ya watu kuvamia eneo hilo na kuendesha shughuli za ujenzi, hivyo kusababisha kuziba kwa njia za maji.”
Ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa si msemaji wa kurugenzi hiyo, anasema kuruhusu ujenzi wa Uwanja kwenye eneo hilo kutasababisha maafa zaidi jijini kutokana na mafuriko.
Ramani ya Uwanja wa Yanga SC

GHARAMA YA KIWANJA JANGWANI
Wakati Yanga ikiwa imekadiria Sh. Bilioni 32 kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja huo, bei ya chini ya kulipa fidia kwa mkazi mmoja mwenye nyumba ya kawaida isiyo ya ghorofa eneo la Jangwani inakadiriwa kuanzia Sh. milioni 700.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa Yanga itahitaji kuhamisha zaidi ya wakazi 30 ambao watalazimika kuwalipa fidia ya Sh. bilioni 21.
Eneo la Jangwani kinavyoonekana kwa ujumla 

WIZARA YA ARDHI
Maofisa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wanasema ni vigumu Yanga kupewa eneo la ziada kwa ajili ya ujenzi huo.
Wanasema kituo cha mabasi yaendayo kasi, ambacho ni cha kudumu, kitajengwa kwenye eneo hilo. 
Rehema Isengo, Ofisa habari wa wizara hiyo, anasema eneo la Jangwani liko katika mipango ya maendeleo.
Eneo hilo licha ya kuwa hatarishi kutokana na kufurika maji kipindi cha mvua, pia ni mkondo wa upumuaji wa bahari na ni bonde ambalo Mto Msimbazi hupita. 
Mabomba ya Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) pia yanapita kwenye eneo la Jangwani, bomba la majisafi likielekezwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na lile la majitaka likielekezwa baharini.
Aidha, Aprili 5, 2011 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka alisema maeneo yote yanayopitiwa na Bonde la Msimbazi kuanzia Daraja la Salender, Muhimbili, Jangwani hadi Vingunguti hayapaswi kujengwa mradi wowote huku akiwataka watu wote waliokuwa wamejenga katika maeneo hayo kuondoka.
Alisema Serikali ina mpango wa kulifanya bonde hilo kuwa eneo la wazi la jiji la Dar es Salaam.
Aliyewahi kuwa kocha wa Yanga SC, Mbelgiji Tom Saintfiet akioongoza wachezaji mazozini Uwanja wa Kaunda mwaka juzi

MANISPAA ILALA
Ombi la Yanga lilijadiliwa katika vikao vya Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Ilala na viongozi wa Yanga waliotaka kushiriki vikao hivyo walizuiwa kuingia ndani ya chumba cha mikutano cha baraza hilo.
Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuitaka Yanga kuwasiliana na ofisi Manispaa ya Ilala, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Severin Assenga alisema mwishoni mwa mwaka kuwa klabu hiyo haiwezi kupewa eneo la ziada Jangwani kwa vile eneo wanalolitaka ni la wazi.
Kwa mujibu wa sheria za ardhi nchini, maeneo ya wazi yanaweza kutumika tu pale panapokuwa na mradi wenye maslahi ya umma na si mtu ama taasisi binafsi.
Francis Kifukwe akizungumza na mkandarasi wa Uwanja wa Kaunda

NEMC WALONGA
Mkurugenzi wa Utekelezaji na Uzingatiaji wa NEMC, Robert Ntakamulenga aliiambia BIN ZUBEIRY mwishoni mwa wiki kuwa ofisi yake ilipata ombi la Yanga na tayari wameiagiza klabu hiyo kufanya tathmini ya athari za mazingira itakayosababishwa na mradi huo.
Baada ya kupokea ombi hilo, anasema wataalam wa NEMC walikwenda kwenye makao makuu ya Yanga na kuonyeshwa eneo linaloombewa kibali cha ujenzi huo.
“Wajumbe wa NEMC) tulikwenda Jangwani tukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (Said Meckysadick) na Mkuu wa Wilaya ya Ilala (Raymond Mushi)  kuangalia eneo ambalo Yanga wanaliombea kibali. Tulishauambia uongozi wa klabu hiyo ufanye tathmini ya athari za mazingira zitakazotokana na mradi huo,” anasema Ntakamulenga.
“Wanatakiwa kufanya tathmini kwa kuwatumia wataalam walioidhinishwa na baraza na sisi (NEMC) tutapitia ripoti na kuangalia kama mradi huo unastahili kupelekwa kwa waziri kwa ajili ya kupatiwa cheti.
“Tunatambua kwamba eneo la Jangwani ni njia kuu ya maji katika jiji hili lakini ripoti ya tathmini ndiyo itatuongoza katika kutoa maamuzi. Kwa sasa hakuna ripoti yoyote iliyoletwa ofisini kwetu kwa ajili ya mradi huo,” anasema zaidi mkurugenzi huyo.
Mwenyekiti wa Yanga SC, Yussuf Manji kulia akiwa na Makamu wake, Clement Sanga

HATI MILIKI JANGWANI
Kifukwe anasema lengo la klabu hiyo ni kujenga Uwanja utakaokuwa na hoteli, kumbi za mikutano, maduka, ofisi, eneo la kuegesha magari na viwanja vingine vidogo kwa ajili ya mazoezi.
Kifukwe anasema Yanga ina eneo lenye ukubwa wa hekta 3.59 ambalo inalimiliki kisheria tangu 1972 na inahitaji eneo lenye ukubwa mara tatu zaidi ya lililopo sasa ili kukamilisha ujenzi huo.
“Kuna watu wamevamia na wanaishi ndani ya eneo letu, baada ya kupatiwa kibali cha ujenzi, itabidi watupishe na tutawaondoa,” anasema Kifukwe na kuongeza:
“Yanga pia italazimika kuingia mfukoni kuwalipa wanaolizunguka eneo la Uwanja wa Kaunda ambalo Serikali itawaongeza ili kufanikisha ujenzi huo.”
Kifukwe anasema mradi huo ambao wameupa jina la ‘Jangwani City’, utalifanya eneo hilo kuwa na mandhari nzuri yenye huduma muhimu kwa wachezaji na wakazi wa maeneo ya jirani.
Tangu kuanzishwa kwake miaka ya 1935 na 1936, klabu kongwe nchini Yanga na Simba zimekuwa zikihaha kusaka viwanja kwa ajili ya mazoezi na mechi za timu zake wakati wa msimu wa ligi na kulazimika kuhamahama mithili ya ndege pori watafutao malisho.
Viongozi wengi wa klabu hizo wamekuwa wakiingia madarakani kwa kuahidi kuipatia suluhu kadhia hiyo kwa kujenga viwanja vya kisasa.
Jumapili Januari 20, mwaka jana uongozi wa Yanga pia ulisema utafanya ukarabati wa jengo la Mafia ili kulifanya kuwa jengo la kitega uchumi huku ukiunda kamati chini ya Mwenyekiti, Ridhiwani Kikwete, lakini Sanga anasema: “Kusimama kwa suala hilo kumetokana na baadhi ya mambo kukwama, kuna nyaraka za umiliki wa jengo hazipo klabuni.”
Mpaka sasa ni klabu mbili, Mtibwa Sugar na Azam FC zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) zenye viwanja vyake binafsi kwa ajili ya mazoezi na mechi za timu zake.
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inasema kujengwa kwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kumeongeza mapato ya Serikali katika sekta ya michezo kwa kiasi kikubwa tangu ulipoanza kutumika rasmi 2007.
Uwanja huo ulijengwa kwa Sh. Bilioni 56 na kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Serikali ya Watu wa China. Tanzania ilichangia Sh. bilioni 25.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KAMATI YA TUZO IMEFANYA MCHUJO KWENYE WACHEZAJI 30 WAMEBAKI 15, MKUDE, AJIBU WAMETOLEWA, ANGALIA ORODHA

Kamati ya Tuzo za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), iliyokutana wiki hii imeteua wachezaji 15 kwa ajili ya kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa VPL msi...

TIBA YA KIIMANI

TIBA YA KIIMANI

a

a
Adbox