KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeamua kuanzia sasa adhabu kwa watu wanaotoa rushwa au kupanga matokeo katika mchezo huo itakuwa ni kufungiwa maisha kujishughulisha na mchezo huo. Taarifa katika tovuti ya TFF imesema kwamba hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo juzi. Kwa muda sasa, kumekuwa na tuhuma nyingi za wachezaji na marefa kuhongwa ili kupanga matokeo- lakini hakukuwa na sheria madhubuti ya kupambana na hali hiyo- lakini kwa hatua hii mpya ya TFF dhahiri itasaidia kupunguza mchezo huo mchafu.
Aidha, baada ya Libya kujitoa kuwa mwenyeji wa Fainali za Afrika (AFCON) za 2017, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limealika nchi wanachama kuomba uenyeji wa fainali hizo.
Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana Agosti 24, mwaka huu imeamua Tanzania kuomba uenyeji wa fainali hizo.
“Tunatambua kuwa moja ya masharti ya kuandaa fainali hizo ni pamoja na nchi kuwa imeandaa moja ya mashindano ya vijana. Lakini kwa kuwa suala hili liko katika mazingira maalumu (exceptional circumstances) tunaamini CAF watafikiria ombi letu kwa msingi huo,”.
Awali Libya ilipewa uenyeji wa fainali hizo 2015, lakini zikahamishiwa Afrika Kusini kutokana na sababu za kiusalama. Hivyo, Libya ikapewa fainali za 2017 ambapo sasa imejitoa yenyewe kuandaa fainali hizo.
Wakati huo huo: Kamati ya Utendaji ya TFF imemteua Boniface Wambura kuwa Mkurugenzi mpya wa Mashindano kuanzia Septemba 1 mwaka huu.
Kabla ya uteuzi huo, Wambura alikuwa Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF kuanzia Januari 1, 2011. Nafasi hiyo sasa iko wazi na itajazwa baadaye na Kamati ya Utendaji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni