Wachezaji wa Simba wakishangilia na kombe lao
WEKUNDU wa Msimbazi Simba chini ya kocha mpya,
Goran Kopunovic wametwaa ubingwa wa kombe la Mapinduzi kufuatia kuifunga Mtibwa
Sugar penalti 4-3 katika mechi ya fainali
iliyopigwa usiku wa kuamkia leo uwanja wa Amaan, Mjini Zanzibar.
Bingwa wa mashindano hayo alilazimika kupatikana
kwa changamoto ya mikwaju ya penalti baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu
pacha ya bila kufungana.
Mashabiki wa kizungu wa msimbazi wakifurahia ushindi wa timu yao jana
Katika kipindi cha kwanza, Simba walianza kwa kasi
wakilisakama lango la Mtibwa Sugar, lakini wakata miwa hao wa Manungu walikuwa
imara kuondosha hatari zote langoni kwao.
Almanusura Emmanuel Okwi aandike goli katika
dakika ya 18, lakini shuti lake lilidakwa na kipa Said Mohammed. Dakika hiyo
hiyo, Ibrahim Hajibu ‘Mido’ aliachia shuti kali ambalo halikulenga lango.
Simba waliendelea kushambulia lango la Mtibwa na
katika dakika ya 21 Jonas Mkude alipiga shuti lililopaa juu ya lango akipokea
mpira wa kona uliochongwa na Okwi na kuguswa kidogo na Salim Mbonde wa Mtibwa.
Shujaa Ivo Mapunda alibebwa na wachezaji wenzake
Dakika ya 23, Hajibu alishindwa kumalizia mpira
uliotemwa na kipa Said Mohammed kufuatia shuti kali liliopigwa na Danny
Sserunkuma.
Beki wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’
alioneshwa kadi ya njano katika dakika ya 27 baada ya kumvuta Ally Shomari.
Hajibu alipoteza nafasi nzuri katika dakika ya 45
akishindwa kumalizia pasi ya Danny.
Mpaka dakika 45 zinamalizika, hakuna timu iliyoona
lango la mwenzako.
Kipindi cha pili Simba waliendelea kucheza vizuri
na kwa kasi na katika dakika ya 56, beki wa kushoto wa Mtibwa, David Charles
Luhend alioneshwa kadi ya njano baada ya kumchezea vibaya Said Hamis Ndemla
Dakika ya 63 beki wa kulia wa Simba, Hassan
Ramadhan Kessy aliachia shuti kali lililogonga mwamba na kuingia tena uwanjani.
Hajib alikwenda kumuona tena kipa Mohammed, lakini
alishindwa kutumia vyema pasi ya Ramadhan Singano ‘Messi’ kufuatia kipa huyo wa
zamani wa Yanga kuudaka mpira.
Kocha Kopunovic alifanya mabadiliko katika dakika
ya 65 akimtoa Hajibu na nafasi yake kuchukuliwa na Elius Mguli.
Kuingia kwa Maguli kuliongeza kasi ya Simba katika
safu ya ushambuliaji.
Katika dakika ya 65, Mtibwa walimtoa Musa Nampaka
na nafasi yake kuchukuliwa na Ibrahim Rajab.
Dakika ya 75 Emmanuel Okwi alikwenda benchi nafasi
yake ikachukuliwa na Awadh Juma.
Musa Hassan Mgosi alioneshwa kadi ya njano katika
dakika ya 78 kufautia kumchezea vibaya Kessy.
Dakika ya 87 Mtibwa walimtoa Ally Shomari na
nafasi yake kuchukuliwa na Ramadhan Kichuya.
Dakika ya 89 Simba walimtoa Ndemla na nafasi yake
kuchukuliwa na Shaaban Kisiga.
Katika dakika ya 90 Mtibwa Sugar walimtoa Ame Ally
na nafasi yake kuchukuliwa na Abdallah
Juma.
Kuhakikisha wanatwaa ubingwa, Simba walimtoa Peter
Manyika katika dakika ya 90 na nafasi yake kuchukuliwa na Ivo Mapunda.
Mapunda ni mzoefu wa kudaka penalti hakuwaangusha
katika mapigo hayo.
Mpaka dakika 90 zinamalizika, hakuna timu iliyoona
lango la mwenzako.
Baada ya hapo mikwaju ya penalti ilifuata na Simba
ndio walikuwa wa kwanza kupiga.
Waliofunga Penalti kwa upande wa Simba ni Awadh
Juma, Hassan Kessy, Hassan Isihaka, Danny Sserunkuma wakati Shaaban Kisiga
alikosa.
Waliofunga kwa upande wa Mtibwa Sugar ni Ally
Lundenga, Shaaban Nditi, , Ramadhan Kichuya, wakati Ibrahim Rajab na Vicent
Barnabas walikosa penalti hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni