Wachezaji wa Simba wakishangilia goli lao
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WEKUNDU wa Msimbazi Simba wametinga fainali ya
kombe la Mapinduzi kufuatia kuibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Polisi
katika mechi wa nusu fainali ya kombe hilo iliyomalizika usiku huu uwanja wa
Amaan Zanzibar.
Bao pekee la ushindi limefungwa katika dakika ya
36 kupitia kwa winga Ramadhan Singano ‘Messi’ akizamisha moja kwa moja mpira wa
adhabu ndogo.
Simba na Mtibwa Sugar zitachuana katika mechi ya
fainali itakayopigwa uwanja wa Amaan Januari 13 mwaka huu.
Simba waliuanza mpira kwa kasi wakipiga mpira wao
wa pasi, lakini mipango iliharibika upande wa kulia kwani beki anayepandisha
mashambulizi Hassan Ramadhan Kessy alipoteza pasi kadhaa alizopewa na Saimon
Sserunkuma.
Safu ya ulinzi ya Simba ikiongozwa na Hassan
Isihaka na Juuko Mursheed katika dakika 10 za mwanzo haikuwa na utulivu wa
kutosha kwani mabeki walichanganyana
mara kwa mara na washambulizi wa Polisi wangekuwa makini wangefumania
nyavu.
Simba waliendelea kufika eneo la wapinzani wao na
katika dakika ya 17 na 18, Kiungo Said Hamis Ndemla alipiga mashuti makali
takribani mita 24 kutoka golini, lakini mlinda mlango wa Polisi, Suleiman Mzee
alifanya kazi nzuri na kuokoa hatari hizo.
Katika dakika ya 26 winga wa kulia wa Simba,
Saimon Sserunkuma alimhadaa beki wa Polisi, Steven Mayala karibu na eneo la
kibendera cha kona, lakini beki huyo alimzuia na mwamuzi akaamuru mpira wa
adhabu ndogo.
Ramadhan Singano ‘Messi’ alikwenda kupiga mpira
huo na ‘guu’ lake la kushoto na gozi la ng’ombe likazama moja kwa moja nyavuni
huku kipa Mzee akiambulia patupu.
Hilo lilikuwa bao la pili kwa Singano kwani
alifunga pia Simba ikishinda bao 1-0 dhidi ya JKU katika mchezo wa mwisho wa
kundi C.
Dakika ya 36, Singano aliingiza krosi murua,
almanusura Saimon acheke na nyavu isingekuwa jitihada za golikipa mzee.
Simba waliendelea kulishambulia lango la Polisi
kama nyuki na katika dakika ya 45, Kessy alimpiga mpira mrefu winga ya kushoto
na kumkuta Danny Sserunkuma aliyemiliki gozi na kupiga pasi nzuri ndani ya eneo
la sita, lakini beki Daniel Joram wa Polisi aliondoa mpira huo na kuwa kona
ambayo haikuzaa matunda.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika,
Simba wanaonolewa na Mserbia Goran Kopunovic walitoka kifua mbele kwa bao 1-0.
Kwa ujumla katika kipindi hicho, Simba walicheza
mpira mzuri wakimiliki kwa asilimia 60 dhidi ya 40 za Polisi.
Winga wa kulia Simon Sserunkuma alikuwa mwiba
mkali kwani alionesha kiwango kikubwa akipiga pasi safi, chenga za uhakika na
krosi kadhaa.
Tatizo la Simba katika kipindi cha kwanza
lilionekana safu ya ulinzi ambapo Mursheed na Isihaka hawakuwa na uelewano
mzuri. Pia Mohammed Hussein na Kessy walifanya makosa mara kwa mara.
Ingawa Polisi walizidiwa kwa vitu vingi, walijitahidi
kushambulia kwa kushitukiza, lakini Mlinda mlango Peter Manyika alifuta makosa
ya mabeki wake kwa kuokoa mipira ya hatari.
Dakika ya 45, Simba walifanya mabadiliko ambapo
Elius Maguli akwenda benchi na nafasi yake ikachukuliwa na Ibrahim Hajibu ‘Mido’.
Dakika ya 46, Danny Sserunkuma alipata nafasi nzuri
baada ya kubaki yeye na golikipa, lakini alishindwa kufumania nyavu akipiga
mpira uliodakwa na kipa Mzee.
Katika dakika ya 47 Polisi nao walimtoa Adam Juma
na nafasi yake ikachukuliwa na Rashid Jumanne.
Dakika ya 56 Polisi walifanya mabadiliko wakimtoa Abdallah
Omary na nafasi yake ikachukuliwa na Mohammed Seif.
Dakika ya 58 Polisi walifanya mabadiliko tena
wakimtoa Samir Vicent na nafasi yake ikachukuliwa na Steven Emmanuel.
Dakika ya 60 Polisi walipata kona, lakini haikuzaa
matunda baada ya kipa Manyika kuudaka mpira huo.
Dakika ya 61 Danny Sserunkuma alipata nafasi
nyingine na kupiga shuti ambalo halikulenga lango.
Simba walifanya mabadiliko katika dakika ya
wakimtoa Singano na kumuingiza Shaaban Kisiga ‘Malone’.
Dakika ya 68 Hajibu alipiga shuti kali kufuatia
kupokea pasi ya Mursheed, lakini kipa Mzee alikoa na kuwa kona ambayo haikuzaa
matunda.
Nyota huyo aliyefunga ‘hat-trick’ katika ushindi
wa Simba wa 4-0 robo fainali dhidi ya
Taifa ya Jang’ombe alipata nafasi ya kutoa pasi kwa Danny, lakini akalazimisha
kupiga shuti ambalo lilikuwa mboga kwa kipa.
Simba walifanya mabadiliko tena katika dakika ya
79 wakimtoa Simon na kumuingiza Awadh Issa Juma.
Wakati huo huo kamati ya mashindano ya kombe la Mapinduzi imemtangaza Said Ndemla kuwa mchezaji bora wa mechi na amekabidhiwa zawadi ya king’amuzi cha Azam TV
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni