Uongozi wa Simba umekasirishwa na kitendo cha Straika wake,
Elius Maguri kupeleka malalamiko dhidi ya klabu kwenye vyombo vya habari.
Mkuu wa Idara ya
habari na Mawasiliano wa Wekundu hao wa Msimbazi, Haji Sunday Manara
amesema sasa imekuwa kama desturi kwa wachezaji wa timu hiyo kukimbilia katika
vyombo vya habari pale wanapohisi hawajatendewa haki.
Manara amesisitiza kwamba Simba itakaa kimya na inataka
kuonesha mfano ikianza na Maguri ambaye ilimsajili mwaka jana kutokea klabu ya
Ruvu Shooting ya Pwani.
“Maguri hana nidhamu, huwezi kwenda kuzungumza kwenye vyombo
vya habari. Sisi tutakaa kimya, atasaidiwa na vyombo vya habari”. Amesema
Manara na kuongeza: “Imekuwa desturi ya wachezaji wa Simba, kidogo tu
wanakwenda kwenye vyombo vya habari, tunataka tutoe mfano, tunaanza na yeye
(Maguri)”.
Katika malalamiko yake, Maguri alisema hajui kinachoendelea dhidi yake kwani amekuwa
akituma ujumbe mfupi wa maandishi kwa viongozi wa Klabu hiyo ikiwa ni pamoja na
kuwapigia simu ikitaka kujua hatma yake, lakini hapati majibu.
Maguri alifafanua kwamba walipotoka Zanzibar ambako waliweka
kambi ya wiki mbili , wachezaji walitakiwa kuingia kambini kujiandaa na mechi
ya Simba Day dhidi ya Sports Club Villa ya Uganda, lakini jina lake halikuwepo.
Kuhusu kuachwa kwenye kikosi kilichoingia kambini kucheza na
SC Vila, Manara amemjibu
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Prisons kwamba: “Ni
utaratibu, kwani lazima awepo kila mahali, mbona wachezaji wengine waliachwa,
kwani yeye ni nani? Sio lazima, ni maamuzi ya kocha”.
Maguri amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake na taarifa
za chini zinasema Kerr hana mpango naye na ameagiza atolewe kwa mkopo au
avunjiwe mkataba.
Kwa miezi kadhaa iliyopita, Simba iliingia kwenye mgogoro wa
kimkataba na winga wake, Ramadhan Singano ‘Messi’ na msingi wake uliibuliwa na
vyombo vya habari.
Singano alidai alisaini mkataba wa miaka miwili mwaka 2013
na ulitakiwa kuisha Julai mwaka huu, lakini Simba wao walisema Winga huyo
alisaini miaka mitatu na ilitakiwa kumalizika Julai 2016.
Shirikisho la soka nchini (TFF) kupitia kamati ya Sheria na
hadhi za wachezaji ndio ilimtangaza Singano kuwa huru kwa kigezo cha Simba
kushindwa kutimiza matakwa ya kimkataba.
Kesi haikuwa idadi ya miaka tena, ikabaki kukiukwa kwa
vipengele vya kimkataba ikiwemo pango la nyumba.
Baada ya kushinda, Singano alisajiliwa na Azam FC siku
chache baadaye.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni