MABINGWA
wa zamani wa Afrika, TP Mazembe, wanatarajiwa kutua nchini kesho ambapo
pamoja na mambo mengine, watawachunguza kwa karibu zaidi nyota kadhaa
waliotamba kwenye michuano ya Kombe la Kagame iliyomalizika wiki
iliyopita jijini Dar es Salaam, wakiwamo Geoffrey Mwashiuya na Malimi
Busungu wa Yanga.
Kwa mujibu wa habari
zilizolifikia gazeti la BINGWA juzi, miamba hiyo ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC), imeonekana kuvutiwa na wachezajihao kutokana na viwango vyao, wakiwamo Pascal Wawa, Mussa Farid na wengineo wa Azam.
Mtu wa karibu na timu
hiyo wanayochezea Watanzania, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu,
alisema kuwa mabosi wa TP Mazembe wamevutiwa na baadhi ya wachezaji wa
Yanga na Azam waliocheza Kagame wakipata picha kuwa Tanzania imesheheni
vipaji vya soka hivyo ni vema wakaelekeza nguvu zao ili kuviendeleza.
“Kombe la Kagame ni neema
kwa wachezaji wa Tanzania, (mabosi wa TP Mazembe) walikuwa wakifuatilia
sana mashindano hayo na kugundua vipaji vingi tu, wakiwamo Busungu,
Geoffrey, Deus Kaseke pamoja na wengine kutoka Azam, wakimtaja pia Wawa
raia wa Ivory Coast,” alisema mtoa habari wetu huyo ambaye hakutaka jina
lake kuwekwa hadharani.
Alisema TP Mazembe
wamebaini kuwa wanaweza kupata wachezaji wenye umri mdogo kutoka
Tanzania na kuwaendeleza kwa maslahi ya klabu yao kama wanavyonufaika na
akina Samatta na baadaye kuwauza Ulaya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni