Na Boniface Wambura, Dar es salaam
Azam
FC ndiyo itakayoiwakilisha Tanzania Bara kwenye michuano ya klabu
bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) iliyopangwa kuanza
Agosti 8 mwaka huu jijini Kigali, Rwanda.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeiteua Azam kuiwakilisha Tanzania
Bara katika michuano hiyo baada ya waandaaji wake, Baraza la Vyama vya
Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kuamua kuindoa Yanga
iliyokuwa icheze awali.
CECAFA
imesema baada ya majadiliano na Yanga kupitia TFF, klabu hiyo ilipewa
muda hadi jana (Agosti 4 mwaka huu) iwe imetekeleza matakwa ya kikanuni
ili iruhusiwe kushiriki michuano hiyo lakini haikufanya hivyo.
Yanga
iliwasilisha orodha ya wachezaji wengi wa kikosi cha pili kwa ajili ya
kushiriki michuano hiyo, jambo ambalo limekatawaliwa na CECAFA kwa vile
linakwenda kinyume na kanuni za michuano hiyo.
Azam
FC ambayo ilishika nafasi ya pili- nyuma ya Yanga katika ligi iliyopita
msimu wa 2012/2013 imekubali kushiriki michuano hiyo na inatarajia
kuondoka nchini kesho (Agosti 6 mwaka huu) kwenda Kigali.
Msafara wa Azam FC katika michuano hiyo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, James Mhagama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni