Mbwana Ally Samatta (kushoto) ameifungia bao la kufutia machozi Taifa stars
HATIMAYE safari ya timu ya Taifa ya Tanzania,
Taifa Stars kuwania tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Africa, AFCON 2015
nchini Morocco imefia mikononi mwa timu ya taifa ya Msumbiji ‘Black Mambas’.
Taifa Stars ikiwa ugenini katika dimba la Taifa la
Zimpeto nje kidogo ya jiji la Maputo imetandikwa mabao 2-1 katika mchezo wa
marudiano wa kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya AFCON
mwakani.
Katika Mechi ya kwanza iliyopigwa wiki mbili
zilizopita jijini Dar es salaam, vijana wa Mholanzi, Mart Nooij walitoka sare
ya mabao 2-2 na leo hii walihitaji kupata ushindi wa aina yoyote ile au sare ya
kuanzia mabao 3-3.
Matokeo ya jumla baada ya mechi mbili, Msumbiji wamefanikiwa kufunga mabao 4 na Taifa
stars matatu, hivyo vijana wa Nooij kutupwa nje ya michuano kwa wastani wa
mabao 4-3.
Msumbiji walikuwa wa kwanza kuandika bao la
kuongoza dakika za mwisho za kipindi cha kwanza kupitia kwa Josimar Tiago
Machaisse, lakini Mbwana Ally Samatta akaisawazishia Stars katika dakika ya 77.
Elias Pelembe ndiye 'mchawi' wa Taifa Stars kwa mwaka huu.
Dakika ya 83, kiungo mshambuliaji wa Msumbiji,
mzoefu, mwenye ujanja mwingi wa kupiga
chenga na kumiliki mpira, Elias Gasper Pelembe aliifungia ‘Domingues’ Msumbiji
bao la pili na la ushindi.
Kihistoria Msumbuji wamemekuwa wababe wa Taifa
Stars inapofika michezo ya mtoano, hasa kufuzu mataifa ya Afrika.
Mwaka 2007 Stars chini ya kocha Mbrazil, Marcio
Maximo ilifungwa bao 1-0 katika mchezo wa mwisho jijini Dar es salaam kuwania
kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2008 nchini Ghana na ingeshinda
ingefuzu.
Bao pekee la Msumbiji lilifungwa dakika ya za
mapema kipindi cha kwanza na aliyekuwa nahodha wake, Tiko Tiko akiunganisha kwa
kichwa krosi nzuri iliyochongwa kutoka winga ya kulia na Elias Pelembe.
Mwaka 2012 Taifa stars ilitolewa tena na Msumbiji kwa
changamoto ya mikwaju ya penati katika mchezo wa kuwania kucheza fainali za kucheza
fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2013 nchini Afrika kusini.
Hatua hii ilifikia baada ya timu hizo kutoka sare
ya bao 1-1 jijini Dar es salaam na kupata matokeo kama hayo mjini Maputo.
Kwahiyo Msumbiji bado wameendelea kuwa wababe wa
Tanzania katika michezo ya mtoano.
Poleni sana Taifa Stars, Poleni Watanzania wote. Mipango mipya inatakiwa kuwekwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni