MABINGWA wa Ulaya Barcelona watatinga Uwanjani bila ya nyota wa Brazil Neymar huku wakisaka kuifikia Rekodi ya AC Milan ya kutwaa UEFA Super Cup mara 5 watakapocheza na wenzao wa Hispania Sevilla ambao ndio waliobeba UEFA EUROPA LIGI Msimu uliopita.
Fainali hii, inawakutanisha Mabingwa wa UEFA CHAMPIONS LIGI ambao ni Barcelona na waliobeba UEFA EUROPA LIGI timu ya Sevilla.
Mchezo huu ni kiashiria cha kuanza rasmi kwa Msimu mpya wa Soka Barani Ulaya chini ya usimamizi wa UEFA na itachezwa kuanzia Saa 3 Dakika 45 Usiku, Saa za Bongo, huko Boris Paichadze Dinamo Arena, Mjini Tbilisi Nchini Georgia.
Mbali ya kumkosa mgonjwa Neymar, ambae nafasi yake itachukuliwa na Pedro anaedaiwa kuhamia Manchester United baada ya Mechi hii, Barca, chini ya Kocha Luis Enrique, pia itawakosa majeruhi Jordi Alba na Douglas huku Wachezaji wapya Arda Turan na Aleix Vidal hawaruhusiwi kucheza hadi Januari kwa vile hivi sasa Barca ipo kwenye Kifungo cha FIFA cha kutosajili Wachezaji wapya.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Sevilla kugombea UEFA Super Cup baada ya kutetea vyema Taji lao la EUROPA LIGI lakini Mwaka Jana kwenye Fainali hii walichapwa 2-0 na Real Madrid.
Sevilla, chini ya Kocha Unai Emery, hawajaifunga Barcelona katika Mechi 19 ingawa safari hii wana nguvu mpya ya Wachezaji wapya Yevhen Konoplyanka na Ciro Immobile. Msimu uliopita katika ligi:- Barcelona 5-1Sevilla , Sevilla 2-2 Barcelona.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni