MSHAMBULIAJI Malimi Busungu leo amekuwa shujaa baada ya kutoa pasi ya bao na kufunga Yanga SC ikiibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Malimi aliyesajiliwa kutoka Mgambo JKT ya Tanga msimu huu, alimpa pasi Amissi Joselyn Tambwe kufunga baada ya kutokea benchi kipindi cha kwanza- kabla ya yeye mwenyewe kufunga la pili kipindi cha pili.
Mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliochezeshwa na refa wa FIFA, Israel Nkongo, hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Tambwe.
Tambwe
alifunga bao hilo dakika ya 44 kwa ustadi mkubwa, akigeuka baada ya
pasi ya Malimi Busungu aliyepokea krosi ya Haruna Niyonzima na
kumchambua kipa Peter Manyika.
Pamoja na kumaliza dakika 45 za kwanza wakiwa wanaongoza, Yanga SC hawakucheza vizuri kipindi cha kwanza na walikoswa mabao mawili ya wazi.
Simba SC walitawala mchezo kipindi cha kwanza na kuwafanya Yanga SC wapoteane kabisa uwanjani, kiasi cha kucheza kwa kujihami muda mrefu zaidi.
Dakika ya kwanza tu, Mwinyi Kazimoto alitia krosi maridadi, lakini mshambuliaji Hamisi Kiiza ‘Diego’ akachelewa na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ akadaka.
Beki Mkongo wa Yanga SC, Mbuyu Twite alifanya kazi nzuri dakika ya tano, baada ya kuokoa krosi nzuri ya beki wa kulia wa Simba SC, Hassan Kessy.
Dakika ya tisa, Nahodha wa Simba SC, Mussa Hassan Mgosi alishindwa kumalizia kazi nzuri ya kiungo Mwinyi Kazimoto na dakika ya 24 Kiiza alifumua shuti kali baada ya pasi ya Said Ndemla na Nahodha wa Yanga SC, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akaokoa.
Shambulizi la kwanza la maana la Yanga SC lilikuja dakika ya 41, baada ya Tambwe kupiga shuti lililokwenda nje akiwa kwenye nafasi nzuri.
Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm alimtoa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, Simon Msuva dakika ya 34 na kumuingiza Malimi Busungu aliyekwenda kuongeza uhai katika safu ya ushambuliaji ya Yanga SC.
Kipindi cha pili Yanga SC walibadilika na kuanza kushambulia moja kwa moja, huku Simba SC nao wakiendelea kuzuia na kusaka bao la pili.
Lakini ni nyota ya vijana wa Jangwani iliyoendelea kung’ara baada ya kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 79 kupitia kwa Busungu aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kurushwa wa Mbuyu Twite.
Baada ya bao hilo, Simba SC walipoteana na kuwaacha Yanga SC kutawala zaidi mchezo.
Kuingia kwa mshambuliaji Msenegali, Pape Abdoulaye N’daw kidogo kuliipa uhai safu ya ushambuliaji ya Simba SC na kuanza kufika langoni mwa Yanga SC, ingawa hawakufanikiwa kupata bao.
Refa Nkongo alimuonyesha kadi ya pili ya njano Mbuyu Twite dakika ya 90+2 kwa kujichelewesha kurusha mpira na Simba SC walitumia dakika hizo za majeruhi kufanya shambulizi moja la maana langoni mwa Yanga SC.
Ushindi huo, unaifanya Yanga SC ijinafasi kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikitimiza pointi 12 baada ya mechi nne, wakati Simba SC inaanza kuporomoka.
Kikosi
cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Mwinyi
Kazimoto, Kevin Yondan, Thabani Kamusoko, Simon Msuva/Malimi Busungu
dk34, Salum Telela/Said Juma ‘Makapu’ dk82, Amissi Tambwe/Deus Kaseke
dk87, Donald Ngoma na Haruna Niyonzima.
Simba SC;Peter Manyika, Hassan Kessy/Pape Abdoulaye N’daw dk84, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murushid, Justice Majabvi, Awadh Juma, Said Ndemla, Hamisi Kiiza, Mwinyi Kazimoto na Mussa Hassan Mgosi/Ibrahim Hajib dk62.
MATOKEO MENGINE
FT | COASTAL UNION | 0 | : | 0 | MWADUI FC |
FT | T.PRISONS | 1 | : | 0 | MGAMBO JKT |
FT | JKT RUVU | 0 | : | 1 | STAND UNITED |
FT | MTIBWA SUGAR | 1 | : | 0 | MAJIMAJI |
FT | KAGERA SUGAR | 0 | : | 0 | TOTO AFRICANS |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni