KIKOSI cha Yanga SC tayari kipo Morogoro tangu asubuhi kwa ajili yake mchezo wake ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania dhidi ya wenyeji Mtibwa Sugar Jumatano.
Yanga SC ambayo Jumamosi iliwazima watani, Simba SC kwa mabao 2-0 ya Amissi Tambwe na Malimi Busungu, imetua Morogoro na kikosi chake kamili kwa ajili ya mchezo.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu watafanya mazoezi Uwanja wa TANESCO leo jioni wakati kesho watafanya Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kwa mujibu wa kanuni ya mgeni kuutumia Uwanja wa mechi siku moja kabla.
Kocha Mhoalanzi wa Yanga SC, Hans van der Pluijm atakuwa peke yake kwa maandalizi ya mchezo huo, kutokana na Msaidizi wake, Charles Boniface Mkwasa kwenda Iringa kwenye msiba wa mama mkwe wake.
Na Yanga SC itamkosa beki wake Mkongo, Mbuyu Twite anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa kwenye mchezo dhidi ya Simba SC Jumamosi.
Mtibwa Sugar wenye maskani yao, Turiani Morogoro wanatarajiwa kuingia Morogoro mjini mapema kesho kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo huo.
Ikumbukwe, Yanga SC na Mtibwa wote wameshinda mechi zao nne za awali na Jumatano kila timu itawania ushindi mwingine ili kumondoa mpinzani kwenye mbio za ubingwa.
Na baada ya Yanga SC kufuta uteja kwa Simba SC Jumamosi, sasa inataka kuvunja mwiko wa kufungwa na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri keshokutwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni