SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesaini mkataba wa miaka mitatu na Kampuni ya Sahara Media wa haki ya kurusha mechi za ligi daraja la kwanza wenye thamani ya shilingi milioni 450 leo.
Akizungumza kwenye hafla ya kusaini mkataba huo, Makamu Mwenyekiti wa Sahara Media, Samwel Nyalla alisema Sahara Media kupitia Star TV itakuwa ikionesha mechi za ligi daraja la kwanza kuanzia msimu.
“Kila mwaka tutatoa milioni 150 kwa miaka mitatu kwa ajili ya haki ya kurusha matangazo ya moja kwa moja ya ligi daraja la kwanza ambayo tayari imeshaanza kuchezwa”, alisema Nyalla
Mkataba huo utazinufaisha timu zinazoshiriki ligi daraja la kwanza ambapo kila timu itapata milioni 15 kila msimu na fedha nyingine zitakazobaki zitakuwa zikilisaidia kuwalipa waamuzi pamoja gharama nyingine za michezo ya ligi hiyo.
Nyalla alisema ligi hiyo itakuwa ikioneshwa kwenye king’amuzi cha continental ambapo malipo yake hayatazidi 10,000 kwa mwezi.
Pia alisema wanatarajia kuzindua chaneli mpya ambayo itafahamika kwa jina la Star Sports Plus ambayo itakuwa inaonesha marudio ya mechi zote za daraja la kwanza na ligi zingine ambayo itakuwa inaonekana kwenye nchi zaidi ya 36 za Afrika.
Naye Rais wa Shirikisho la Soka, (TFF) Jamal Malinzi alimshukuru Nyalla na uongozi wa Sahara Media kwa kukubali kuonesha ligi daraja la kwanza kwani itasaidia kukuza soka kwa kuibua mamalamiko ya waamuzi, wachezaji na viongozi pia itasaidia kuwatangaza wachezaji nje.
“Ligi ikiwa inaoneshwa itasaidia kuuza wachezaji nje kwani mawalaka watakuwa wanafuatilia na kupunguza au kumaliza malalamiko juu ya waamuzi”, alisema Malinzi
Malinzi ameviomba vilabu vya FDL kutumia udhamini huo kama chachu ya mafanikio na kufanya vizuri katika ligi hiyo itakayotoa timu tatu za kupanda Ligi Kuu ya Vodacom (FDL) msimu ujao.
Aidha Malinzi amewaomba wamiliki wa viwanja vinavyotumika kwa michezo ya FDL kuviweka katika hali nzuri ya matunzo ili mechi zinazochezwa katika viwanja hivyo ziweze kuwa nzuri kiufundi na muonekano wa kwenye Luninga.
Mkataba huo ni wa pili kusainiwa na TFF baada ya awali kusaini mkataba na kampuni ya Star Times wenye thamani ya milioni 900.
Jumla ya thamani ya mikataba yote miwili (Star Times pamoja na Sahara Media) ya udhamini wa ligi daraja la kwanza inafikia jumla ya shilingi billioni 1.35.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni