TANZANIA imeporomoka katika viwango vya mchezo wa netiboli duniani baada ya kuondolewa katika orodha ya nchi zinazotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Netiboli (INF), sababu kubwa ikiwa ni kushindwa kucheza michezo mingi ya kimataifa.
Kabla ya viwango hivyo vya sasa vilivyotolewa Oktoba 13, Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 15 kwa muda mrefu, lakini baada ya kushindwa kucheza mechi nyingi za kimataifa, imeondolewa kabisa katika orodha ya nchi 32.
Kwa mujibu wa viwango hivyo vilivyotolewa na INF, Tanzania imo katika orodha ya nchi 11 ambazo zinaweza kurejeshwa katika viwango hivyo vya ubora endapo tu itacheza mechi nane za kimataifa.
Mbali ya Tanzania, nchi nyingi zinazopaswa kucheza mechi nane ili ziweze kurejeshwa katika orodha ya viwango vya ubora ni Argentina, visiwa vya Cayman, Gibraltar, India, Maldives, Pakistan, Taipei, Malta, Vanuatu na Togo.
Australia ndiyo inayoongoza kwa ubora ikifuatiwa na Zew Zealand, England, Jamaica huku Afrika Kusini ikiwa ya tano, lakini ni ya kwanza katika Afrika kwa ubora.
Malawi inashika nafasi ya pili Afrika na Uganda ni ya tatu kwa ubora barani Afrika. Kwa muda mrefu Tanzania ilikuwa inaizidi Uganda kwa ubora, lakini kwani kwa kushindwa kushiriki katika michuano mbalimbali, imejikuta ikikwama katika viwango vya ubora na kupinduliwa.
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Chaneta, Anna Kibira alisema watahakikisha wanacheza mechi nyingi za kimataifa ili kurejea katika viwango vya mchezo huo duniani.
Alisema hakuna sababu inayowazuia kucheza mechi za kimataifa na kurejeshwa katika viwango hivyo, ambapo alisisitiza Desemba watatoa kalenda itakayoonesha mechi za kimataifa watakazocheza mwakani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni