NI ukweli uliowazi kwa sasa kuna ubishi kati ya pande mbili
za timu hasimu Bongo; Simba na Yanga juu ya timu gani ina straika mkali kuliko
nyingine.
Yanga wao wanajivunia uwepo wa Mzimbabwe wao, Donald Ngoma
na Mrundi, Amissi Tambwe ambao hakika wamekuwa chachu ya ushindi kikosini hapo tanngu
kuanza kwa msimu huu, lakini kwa Simba wanaonekana si lolote kwani silaha yao
ni Ibrahim Ajib na Mganda, Hamisi Kiiza.
Ukweli mastaa wote unafanya poa na wamekuwa nguzo muhimu mpaka
sasa ambapo kila timu ina nafasi ya kutwaa ubingwa wa msimu huu, ubora wao
ukianzia kwenye vita ya kusaka ufungaji bora Ligi Kuu Bara mpaka sasa, ambako chati
hiyo inaongozwa na Kiiza mwenye mabao 19, anafuatiwa na Tambwe kwa mabao 17 na
wengine wanafuatia.
Championi imekata mzizi wa fitina na kura imeangukia kwa
Kiiza kama fowadi bora tangu kuanza kwa msimu huu, huku Ngoma licha ya
kuonekana mkombozi wa Wanajangwani, bado anasubiri hata kwa staa wa Azam, Kipre
Tchetche.
Miongoni mwa vigezo vilivyozingatiwa ni wingi wa mabao na uwezo
wa mchezaji katika kuchana nyavu bila kujali ni aina gani ya michuano, kura
iliyowadondokea Kiiza, Kipre na Tambwe, lakini bado Kiiza anabaki juu katika
wingi wa mabao kama mchanganuo wa ‘Top 5’ ya watupiaji bora.
Jeremiah Juma
Fowadi wa Tanzania Prisons anashika nafasi ya tano katika
mafowadi bora mpaka sasa akiwa na mabao 11 katika michuano miwili aliyocheza;
ligi kuu na Kombe la FA. Idadi hii imewashinda mastaa kibao wa Azam, Simba na
Yanga wakiongozwa na Allan Wanga, Ibrahim Ajib, Danny Lyanga, Malim Busungu na
Simon Msuva.
John Bocco, Ngoma
Nahodha wa muda mrefu wa Azam, John Bocco yupo ‘rank’ moja
na Mzimbabwe, Donald Ngoma wa Yanga, wote wakiwa idadi sawa kwa mabao 15 kwenye
michuano yote mitano waliyocheza msimu huu.
Lakini kwa kigezo cha fowadi
asiyechagua michuano, Bocco ni bora ya Ngoma kwani katika michuano mitano
amefunga katika michuano minne mpaka sasa (ligi kuu mabao (8), Mapinduzi (2),
Kombe la Shirikisho (2) na Kagame (2).
Ngoma katika michuano mitano ambayo Yanga imehusika msimu
huu, amefanikiwa kufunga kwenye miwili tu; ligi kuu (13) na Ligi ya Mabingwa
Afrika mabao mawili.
Kipre Tchetche
Ni wa tatu katika chati ya mafowadi bora mpaka sasa akiwa na
mabao 17. Staa huyo wa Azam wikiendi iliyopita alidhihirisha ubora wake baada
ya kupachika mabao matatu katika ushindi wa mabao 4-3 waliyovuna Azam mbele ya
Wasauz, Bidvest na kutinga hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho.
Katika michuano mitano ambayo Azam imehusika msimu huu,
Muivory Coast huyo amefunga katika michuano minne (ligi kuu (mabao 9),
Mapinduzi (1), Kagame (4), Shirikisho (4).
Amissi Tambwe
Heshima yake kubwa ni kupiga hat trick, anazo tano za ligi
kuu katika misimu mitatu aliyokaa Bongo hii. Anashika nafasi ya pili akiwa
amefunga mabao 20 katika michuano mitano ambayo Yanga imeshiriki msimu huu.
Katika michuano hiyo, Mrundi huyo amefanikiwa kufunga katika michuano minne
ambayo ni ligi kuu mabao 17, Mapinduzi (1), Kagame (1) na Ligi ya Mabingwa (1).
Hamisi Kiiza;
Kuna rundo la sababu za kumfanya kuwa fowadi bora mpaka
sasa. Kwanza ndiye mwenye mabao mengi tangu kuanza kwa msimu huu ambako
amefunga mabao 23, mabao matatu zaidi ya anayemfuatia, Tambwe.
Pili, kati ya orodha ya wakali watatu wa juu, ndiye aliyeshiriki
michuano michache zaidi. Mitatu tu, Kombe la FA, ligi kuu na Mapinduzi ambapo
amefunga kwenye ligi kuu mabao 19 na manne kwenye FA, kwa mantiki iwapo
angeshiriki mitano kama kina Ngoma na Kipre pengine angekuwa anachungulia mabao
30 kwa sasa.
Tatu, katika orodha hiyo, Kiiza pekee ndiye amefunga kwenye
Kombe la FA tena akifunga mabao mawili-mawili kila mchezo mpaka Simba inatinga
robo fainali.
Hitimisho:
Kiiza anahitaji bao moja tu katika mechi sita za ligi kuu
Simba ilizobakiza ili kuandikisha rekodi ambayo haijawahi kutokea kwenye soka
la Tanzania. Bao hilo litamfanya kufikisha mabao 20, idadi ambayo kwa mujibu wa
takwimu, hakuna mchezaji wa kigeni aliyewahi kuifikisha .
Mkenya, Boniface Ambani wa Yanga msimu 2008/09 alitwaa kiatu
kwa mabao 18, Tchetche wa Azam 2012/13 alikuwa na mabao 17 wakati Mrundi Tambwe
ndiye mwenye mabao mengi, alipokitwaa akiwa na mabao 19 msimu wa 2013/14 akiwa
na Simba.
Kiiza atakuwa Mganda wa pili kuwa mfungaji bora baada ya Michael
Katende wa Kagera Sugar afanye hivyo 2007/2008 alipomaliza ligi na mabao 11.
www.mdosejr@gmail.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni