Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WEKUNDU wa Msimbazi, Simba wamelazimisha sare ya
mabao 2-2- na Wagosi wa Kaya, Coastal Union katika mchezo wa ufunguzi wa ligi
kuu soka Tanzania bara uliomalizika jioni hii uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Simba chini ya kocha Patrick Phiri walianza mpira
wakilishambulia mara kadhaa lango la Coastal na katika dakika ya 7 ya kipindi
cha kwanza Mnyama aliandika bao la kuongoza kupitia mpira wa adhabu ndogo
uliopigwa na kiungo mkongwe, Shaaban Kisiga ‘Malone’.
Katika kipindi hicho cha kwanza, Simba waliendelea
kucheza vizuri kuanzia safu ya kiungo ambapo Piere Kwizera na Kisiga walionekana
kupiga pasi za uhakika, lakini haikuwa rahisi kupasua ngome ya Coastal.
Mara kadhaa Singano na Chanongo walipiga krosi
kutoka pande zote za kulia na kushoto, lakini Amissi Tambwe na Okwi walishindwa
kukaa maeneo sahihi.
Mnamo dakika ya 36, Tambwe aliandika bao la pili
kwa njia ya kichwa akiunganisha krosi iliyochongwa na Okwi kutoka winga ya kulia na kumuacha kipa wa Coastal
Union Shaaban Kado akiokota manyoya.
Dakika ya 56, Uhuru aliingia akitoke benchi
kuchukua nafasi ya Haruna Chanongo.
Phiri alifanya mabadiliko ambapo katika dakika ya
64 Tambwe alikwenda benchi na nafasi
yake ilichukuliwa na Paul Kiongera.
Wakicheza kwa nguvu na kuonekana kushambulia
zaidi, huku wakipiga mashuti matano
yaliyolenga lango, Coastal walionekana kucheza kwa nguvu, wakitawala
mpira sehemu ya kiungo na kuwafanya Simba wasicheze mpira wao.
Wakati Simba wakihangaika kuwakaba washambuliaji
wa Coastal, dakika ya 66, Lutimba Yayo Kato aliwafungia Wagosi wa kaya bao la
kwanza la kusawazisha.
Wakiendelea kuwa katika ubora wao kwa kipindi
hicho cha pili, Ramadhani Salim aliwasawazishia Coastal bao la pili katika
dakika ya 82 kupitia mpira wa adhabu ndogo.
Kwa ujumla kipindi cha pili Coastal Union
walicheza kwa kiwango cha juu na kuwazidi ujanja wachezaji wa Simba.
Simba dhahiri hawana kiungo wa ukabaji kutokana na
kukosekana kwa Jonas Mkude.
Mabeki wa kati, Joseph Owino na Hassan Isihaka
mara nyingi walikosa mtu wa kuwasaidia kupunguza kasi ya washambuliaji wa
Coastal Union na kujikuta wakifanya makosa kadhaa yaliyowagharimu.
Kwa bahati mbaya, Messi na Chanongo sio wazuri
sana pale timu inapokosa mpira na ndio maana safu ya ulinzi ya Simba haikuwa na
msaada mkubwa kutoka safu ya kiungo wakati ikiwa imezidiwa.
Katika mchezo huo, Simba walipata kona tatu sawa
na Coastal Union, wakati huo huo Mnyama aliotea mara 10 wakati Coastal wao
waliotea mara tano.
Ligi hiyo itaendelea wikiendi ijayo (septemba 27
na 28 mwaka huu).
Septemba 27, Simba watakuwa nyumbani uwanja wa
Taifa kuchuana na Polisi Morogoro iliyofungwa mabao 3-1 jana na Azam fc katika
uwanja wa Azam Complex.
Coastal Union watasafiri mpaka uwanja wa Sokoine
Mbeya kukabiliana na Mbeya City fc iliyotoka suluhu (0-0) jana dhidi ya JKT
Ruvu katika uwanja huo.
Mtibwa Sugar walioshinda 2-0 dhidi ya Yanga jana uwanja
wa Jamhuri Morogoro watakuwa nyumbani Manungu kuchuana na Ndanda fc walioshinda
mabao 4-1 jana dhidi Stand United katika uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga.
Azam fc walioshinda 3-1 jana dhidi ya Polisi Morogoro
watakuwa nyumbani tena Azam Complex kuoneshana kazi na Ruvu Shootings
iliyotandikwa 2-0 na Prisons jana uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani.
Mgambo JKT walioshinda jana 1-0 dhidi ya Kagera
Sugar siku hiyo watakuwa nyumbani CCM Mkwakwani Tanga kuwakabili Stand United
waliotandikwa na Ndanda fc.
Septemba 28 mwaka huu, JKT Ruvu wakitokea kuambulia
0-0 na Mbeya City jana Sokoine wataikabili Kagera Sugar iliyochapwa 1-0 jana na
Mgambo JKT.
Yanga wakiwa na machungu ya kufungwa 2-0 na Mtibwa Sugar, wataikaribisha Prisons iliyotoka kushinda jana Mabatini na mechi hiyo itapigwa uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni