RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amewaahidi Sh. Milioni 1 kila mchezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars iwapo watashinda mchezo wa kwanza raundi ya kwanza kufuzu michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), dhidi ya Uganda.
Taifa Stars watakuwa wenyeji wa Uganda ‘The Cranes’ leo Uwanja wa Amaan visiwani hapa katika mchezo wa kwanza wa michuano hiyo ya CHAN, inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye mjini Kampala.
Na Malinzi amezungumza na wachezaji jana jioni Uwanja wa Amaan kuelekea mchezo wa leo na kuwaahidi iwapo watashinda, mbali na posho za kawaida za kambi, atawapa Milioni 1 kila mmoja.
“Watu wanataka ushindi, matusi yote kwa TFF, huyo Malinzi anatukanwa kila sehemu. Nyinyi wenyewe mnatukanwa, mnapiga mawe. Kwa kweli hali na mbaya.
TFF tumejitahidi kuwafanyia kila kinachostahili na tutaendelea kuwafanyia, ni jukumu letu na hakuna siku tumewanyima, tungekuwa na posho zaidi, tungewapa,”amesema Malinzi na kuongeza;
“Lakini sisi tunafanya mambo yetu nje ya Uwanja, mkikanyaga uwanjani ni nyinyi, Bocco...kapaisha, Ndemla kapigwa chenga..dhidi ya Uganda ni vita kubwa haijawahi kuonekana, Waganda mnawajua, Cannavaro mjitahidi kukimbizana nao, msicheze kama mpo ugenini, pambaneni kwa kujiamini, mpo nyumbani.”amesema.
Kwa upande wake, Nahodha wa Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema kwamba watajitahidi kulipigania taifa leo na kwamba wako tayari kwa mpambano.
Jumla ya wachezaji 21 wapo kambini Zanzibar hoteli ya Nungwi Inn na maana yake bila kuhusisha watu saba wa benchi la ufundi, Malinzi atalazimika kutoa Sh. Milioni 21 iwapo Stars itashinda leo.
Wachezaji waliopo kambini wanao tarajiwa kucheza siku ya leo ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ na Mwadini Ali, mabeki; Mwinyi Haji Mngwali, Hassan Isihaka, Shomary Kapombe, Oscar Joshua, Salum Mbonde, Aggrey Morris na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Viungo ni; Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Abdi Banda, Frank Domayo, Amri Kiemba, Said Ndemla, Hassan Dilunga na Kelvin Friday wakati washambuliaji ni; Atupele Green, Rashid Mandawa, Simon Msuva na John Bocco.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mholanzi Mart Nooij amesema vijana wake wako katika hali nzuri kuelekea kwenye mchezo dhidi ya Uganda.
Stars inahitaji ushindi katika mchezo huo wa awali ili kujiweka katika mzingira mazuri ya kusonga mbele, kabla ya mchezo wa marudaino utakaofanyika baada ya wiki mbili jijini Kampala.
Lakini pia ushindi utarejesha imani ya wananchi baada ya timu kufungwa mechi nne mfululizo- ikiwemo iliyopita ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) walipofungwa 3-0 na Misri mwishoni mwa wiki mjini Alexandria.
Stars ikiitoa Uganda itacheza na Sudan na mshindi wa mchezo huo moja kwa moja atafuzu CHAN 2016 nchini Rwanda.
Mwaka jana, Tanzania ilitolewa na Uganda katika mechi za kufuzu CHAN.
Waaamuzi wa mchezo huo kutoka Rwanda Hudu Munyemana, Hakizimana Ambroise, Justin Karangwa na Issa Kagabo tayari wamewasili Kamisaa Nicholaus Musonye kutoka Kenya
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni