SHIRIKISHO la Soka Tanzania(TFF) limetangaza kujiunga na Asasi ya GSI kwa ajili ya kuweka barcode (msimbomilla) au alama hiyo kwenye jezi za timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ili kuwa rahisi kudhibiti mapato na uuzaji holela wa bidhaa hizo.
GSI ni Shirika la Kimataifa linalojihusisha na udhibiti wa bidhaa zinazozalishwa, ambapo Tanzania ni mwanachama kwa namba 620 tangu mwaka 2011 wakifanya kazi na zaidi ya makampuni 780 .
Akizungumza leo na waandishi wa habari Rais wa TFF Jamal Malinzi alisema wamejiunga na GSI ili kupata alama hiyo itakayowasaidia kudhibitiza wizi lakini pia, uuzwaji holela wa jezi hizo.
“Tunaamini alama ya GSI ikiwapo katika jezi tutakomesha watu ambao wamekuwa wakiuza jezi feki, na wale wote wenye makontena Kariakoo, wajue kuwa sasa tutauza zile zenye alama hii, tupate mapato yetu kwa manufaa ya Shirikisho,”alisema.
Alisema hata klabu kama zinahitaji kudhibiti mapato yao, ni muhimu zikajiunga huko kuwekewa nembo hiyo kwenye jezi.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa GSI, Fatma Kange alisema jezi ikiwa na alama (barcode) itauzwa popote katika maduka mbalimbali makubwa kwa vile itakuwa na nembo inayojulikana kimataifa.
Alisema watafurahi pia, ikiwa watapewa nafasi katika kuweka alama hizo kwenye tiketi za kuingilia uwanjani, kwani kazi yao ni kubwa huku akisema hata vyuo vikitaka kujua ni kwa jinsi gani watapambana na wanafunzi wasiolipa ada wanasuluhisho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni