RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi amesema Kocha Mkuu wa timu ya Taifa Mart Nooij akishindwa kuivusha timu katika michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) kibarua chake kitaota mbawa.
Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku chache zimepita baada ya kpcha huyo kunyooshewa vidole na wadau wa soka kwa kushindwa kufanya vizuri kuanzia kwenye michuano ya Baraza la Vyama vya soka Kusini mwa Afrika (COSAFA) na mchezo dhidi ya Misri kufuzu michuano ya Afrika uliochezwa juzi.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari leo Malinzi alisema Nooij alipewa muda wa kuhakikisha anaivusha Taifa Stars katika michuano ya CHAN, na kwamba baada ya kurejea atajiandaa kwenda Zanzibar kwa ajili ya mchezo wa CHAN wa kwanza dhidi ya Uganda.
“Kamati ya Utendaji ya TFF ilimpa Kocha jukumu la kuivusha Tanzania katika michuano ya CHAN, tunataka kushiriki michuano hii itakayofanyika nchini Rwanda,” alisema.
Baada ya mchezo huo wa Jumamosi, mchezo wa marudiano dhidi ya Uganda utachezwa Julai 4, mwaka huu nchini Uganda.
Baadhi ya wadau wa soka wamekuwa wakipendekeza kufukuzwa kwa Kocha huyo wakidai kuwa ameshindwa kusaidia timu hiyo.
Miongoni mwa wadau hao ni Rais wa zamani wa Simba Ismail Rage, ambaye ameonyesha kukerwa na matokeo mabovu ambayo Taifa Stars imekuwa ikiyapata na kupendekeza umuhimu wa kutimuliwa kwa Kocha huyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni