Katibu Mkuu wa Coastal Union,Kassim El Siagi akiwaonesha
wanahabari baadhi ya vifungu vya mkataba wa Banda wakati wa mkutano na wanahabari jana klabuni Coastal Union.
UONGOZI wa Klabu ya Coastal Union ya Tanga umekiri kupokea barua kutoka kitengo cha
Wanasheria (Maleta & Ndumbaro Advocate cha Dar) ikisema kuwa timu hiyo imeshindwa kumlipa Abdi Banda mshahara
wa miezi mitatu mfululizo na kusema imevunja mkataba.
Akizungumza jana,Katibu wa Coastal Union,Kassim El Siagi amekanusha
na kuwa habari zilizoenezwa kwamba walishindwa kumlipa mshahara
mchezaji huyo sio za kweli bali kilichotokea ni kwamba Banda
alifundishwa na watu wajinga asichukue mishahara yake ya miezi
mitatu ili kukipa hadhi kipengele hicho cha sheria kilichopo kwenye
mkataba wake,
“Akinukuu kipengele cha ibara ya 3(3.2)(1) cha mkataba wa Banda
kinachosema kuwa ikiwa klabu imeshindwa kumlipa mchezaji mishahara
yake ya miezi mitatu mfululizo basi mkataba wa mchezaji huyo na klabu
umevunjika “Alisema El Siagi.
Alisema alichokifanya mchezaji Banda ni kukwepa kuchukua
mishahara yake makusudi ili ionekane kwamba hakulipwa miezi mitatu .
El Siagi alisema alichokifanya ni mambo mawili, jambo la kwanza ni
kudanganya wanamichezo hapa nchini na klabu yake ya Coastal Union ili
aipatie fedha Klabu ya Simba ambapo huo ni Wizi wa kutumia hila.
Alisema la pili ni kitendo cha kusaini mkataba Simba wakati akijua ana
mkataba na Coastal Union ambao unatarajiwa kuishia Juni 2016.
Katibu huyo alisema ni makosa makubwa mchezaji huyo kusaini mikataba
miwili tofauti katika kipindi cha msimu mmoja kwa sababu atakuwa
amevunja taratibu za mikataba kutokana na kuwa mchezaji hawezi kuwa na mikataba
miwili kwa wakati mmoja.
Aidha alisema kutokana na mchezaji huyo kudanganya na kukiuka
utaratibu wa mkataba, Uongozi wa Coastal Union umejipanga kumchukulia hatua
kali mchezaji huyo ikiwemo hatua za kinidhamu.
Katibu huyo alisema anashangazwa kuona kuwa klabu ya Simba yenye
viongozi wazoefu kwenye masuala ya mpira wanafanya makosa kama hayo
kwa kutokufuata taratibu za kiusajili.
“Kanuni za shirikisho la soka Dunia (FIFA) na Shirikisho la soka
nchini (TFF) zinasema mchezaji hawezi kuzungumza na timu yoyote wakati akiwa
ndani ya mkataba mpaka labda awe amebakiza miezi sita kwenye mkataba wake ndio
anaruhusiwa kuzungumza na uongozi wa klabu nyingine.
Aliongeza kuwa iwapo mchezaji akiwa amebakiza mwaka mmoja basi klabu na klabu
ndio zinaruhusiwa kuongea na sio mchezaji hivyo Banda bado ana miaka miwili
Coastal Union ambayo imebaki hivyo Simba
walichotakiwa kufanya ni kuzungumza na uongozi wa Coastal union ili
kumnunua mkataba wake badala ya kurubuniwa na kauli hafifu za
kiudanyanyifu.
Katibu huyo alisema kwa kufanya hivyo Coastal Union kupitia wanasheria
wake ,Divine Chambers Advocates & Hamidu Mbwezeleni wanajipanga
kuwaandikia barua shirikisho la soka nchini (TFF) pamoja na Simba ili
kudai fidia ya ukiukaji wa taratibu hizo.
Alieleza kuwa tayari Coastal Union wamemtumia mwanasheria wa Banda
majibu ya barua yake kupitia mwanasheria Divine Chambers Advocates ya
Mjini Tanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni