Washtakiwa
watatu wanaokabiliwa na mashtaka ya mauaji dhidi ya mtoto Nasra Rashid
Mvungi, wamelazimika kubadilishiwa hakimu baada ya hakimu wa awali,
kupata dharura na kutokuwepo mahakamanani hapo.
Washtakiwa
hao ambao kesi yao imekuwa ikifikishwa na kutajwa, mbele ya hakimu
mkazi mfawidhi wa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Morogoro, Mary Moyo,
walilazimika kupandishwa kizimbani mbele ya hakimu Agripina Kimanze na
kusomewa mashtaka yao, baada ya hakimu moyo kutokuwepo mahakamani,
ambapo tofauti na nyakati zingine, shauri hilo lilichelewa kuanza.
Mwendesha
mashtaka wa polisi Aminatha Mazengo, akisoma shitaka, aliiambia
mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kwamba
jalada bado lipo kwa mwanasheria mkuu wa serikali, hivyo kuiomba
mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Mahakama
iliridhia ombi hilo, na kupanga Agosti 20 mwaka huu, kufikishwa tena kwa
kesi hiyo kwaajili ya kutajwa, kutokana na mahakama hiyo kukosa uwezo
kisheria kusikiliza shitaka la mauaji na washtakiwa kurudishwa rumande
kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana.
Kesi hiyo
ya mauaji inawakabili washitakiwa watatu akiwemo baba mzazi wa mtoto
Nasra, bw. Rashid Mvungi pamoja na waliokuwa walezi wake, Bi Mariam Said
na mumewe Mtonga Omary, ambao awali walikuwa wakikabiliwa na shitaka la
kula njama na kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto Nasrah Mvungi
kabla ya baadaye mashitaka yao kubadilishwa na kuwa ya mauaji baada ya
mtoto huyo kufariki dunia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni