Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Licha ya kuajiri watendaji wapya
wenye weledi, Yanga SC imekubaliana na wazo la baadhi ya wanachama wake
kusomwa dua maalum kuondoa nuksi katika kikosi chao.
Hivi karibuni Yanga SC ilitangaza kuwatimua baadhi ya watendaji wake na
kuajiri wataalam wapya wakiwamo mtangazaji wa zamani wa ITV na TBC,
Jerry Muro ambaye pia aliibuka mwandishi bora wa habari wa mwaka pamoja
na Daktari wa Michezo, Jonas Tiboroha.
Lakini, Yanga SC leo imeamua kusahau weledi wa watendaji wake wapya na
kuridhia wazo la kusomwa kwa dua ili "kuondoa mikosi kwenye kikosi cha
Jangwani."
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Muro amesikika
katika Kipindi cha 'Spoti Leo' cha Radio One Stereo usiku huu akisema:
"Hawana kizuizi na wanachama wao wanaotaka isomwe dua kuondoa mikosi
kikosini."
Ikumbukwe kuwa Yanga SC licha ya kuwa na wachezaji wakali wakiwamo
watano wa kimataifa, Warwanda Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite, Mliberia
Kpah Sherman, Mbrazil Andrey Coutinho na Mrundi Amisi Tambwe imeshindwa
kung'ara katika michuano ya Kombe la Mapinduzi ikifungwa 1-0 na JKU na
haina matokeo mazuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL)
ikiwa nafasi ya nne baada ya kubanwa na Ruvu Shooting Jumamosi.
"Watu wanasema sisi tumeingia wa kisasa, lakini Bakiri Makele
(Mwenyekiti wa Vijana wa Yanga SC) na wenzake wanasema na wamelifanyia
ufafanuzi MZURI suala hilo. Timu hii ni ya wanachama, si ya Jerry Muro
na Tiboroha.
"Tuko tayari jambo lolote lifanyike klabuni mradi liwe na maslahi ya
timu na ustawi wa klabu. Kuna tofauti ya kutambika na kusoma dua. Sisi
tunataka kusoma dua na si kutambika. Makele ameeleza vizuri kuhusu suala
hili," amesema Muro.
Katika hatua nyingine, Muro amesema timu yao leo asubuhi imefanya
mazoezi mepesi Uwanja wa Kawe na itaingia kambini kesho Bagamoyo na
keshokutwa majira ya mchana wataanza safari kwenda Morogoro, tayari
kumenyana na maafande wa Polisi Moro Uwanja wa Jamhuri mjini humo
Jumamosi.
Kuhusu afya ya mchezaji kiraka Mbuyu Twite, Muro amesema Mrwanda huyo
mwenye asili ya DRC ameimarika kiafya na kuna uwezekano mkubwa wa kwenda
naye Mji Kasoro Bahari.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni