Kiungo wa Simba SC anaye kipiga kwa mkopo kwenye klabu ya Stand United Haruna Chanongo ameitwa kwa ajili ya majaribio ya wiki mbili kwenye klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mkurugenzi wa benchi la ufundi wa Stand United Muhibu Kanu amesema, wamepokea taarifa kutoka uongozi wa klabu ya TP Mazembe ya kumuhitaji Haruna Chanongo kwa ajili ya majaribio ya muda wa wiki mbili na kama atafuzu basi atajiunga na mabingwa hao wa zamani wa Afrika.
“Tumepokea taarifa kutoka TP Mazembe wakimuhitaji Chanongo anayecheza hapa kwa mkopo kwa ajili ya majaribio ya wiki mbili. Wamehitaji picha za video za mchezaji huyo na tayari tumesha watumia video mbali mbali za Chanongo akiwa Simba, Stand na timu ya Taifa ‘Tifa Stars’,” amesema Kanu.
“Uongozi wa Stand United umemruhusu Chanongo kwenda TP Mazembe kwa ajili ya majaribio na atakwenda huko kabla au baada ya mechi yetu dhidi ya Yanga tarehe 7 Machi mwaka huu,” Kanu akaongeza.
Lakini Kanu akaongeza kuwa hiyo ni nafasi kwa Chanongo kuweza kuonesha kipaji chake na kucheza soka la kulipwa kwenye vilabu vikubwa Afrika na baadae hata Ulaya.
Kama Chanongo atafuzu kwenye majaribio hayo na kufanikiwa kujiunga na TP Mazembe atakua mchezaji wa tatu kujiunga na klabu hiyo kutoka Tanzania akiungana na Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta ambao wanacheza kwenye klabu hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni