Kuelekea kilele cha siku ya Simba Day inayoadhimishwa kila ifikapo Agosti 8, uongozi wa klabu ya ‘wekundu wa Msimbazi’ Simba umetangaza mabadiliko ya timu ambayo itacheza na Simba SC kwenye mechi ya kirafiki ya kujipima nguvu tofauti na ilivyokuwa awali ambapo Simba ingecheza na A.F.C Leopards ya Kenya lakini sasa itamenyana na Sports Club Villa ya Uganda.
Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba Said Tully amefafanua ni kwanini watacheza na Sports Club Villa na sio A.F.C Leopards kama ilivyokuwa imetangazwa mwanzo. Tuli amesema klabu ya A.F.C Leopards inamgogoro hivyo haitaweza kuja tena na wameona busara kuialika timu ya SC Villa ya Uganda katika mchezo huo wa kirafiki.
“Maandalizi yapo vizuri lakini kwa bahati mbaya au nzuri ni kwamba, hatutacheza tena na A.F.C Leopards, tutacheza na Sports Club Villa ya Uganda ambayo inatarajiwa kuwasili leo (Alhamisi) na kufanya mazoezi yake katika uwanja wa Karume baada ya hapo timu hiyo itafanya mazoezi tena siku ya Ijumaa (kesho) kuelekea mechi ya Jumamosi”, amesema Tuli.
“Hayo ni mabadiliko ambayo yametokea baada ya timu ya A.F.C Leopards ya Kenya kukosa ruhusa kutoka chama cha mpira cha Kenya lakini pia timu hiyo ipo kwenye mgogoro na baadhi ya wachezaji akiwemo pia kocha wao, wamegoma kuwepo kwenye timu hiyo”.
“Kwahiyo tukaona tunaweza kujiingiza kwenye matatizo ambayo mwisho wa siku tukaonekana tumefanya kitu ambacho kiko tofauti na watu wanavyotarajia na ndio maana tukaamua kuongea na timu ya Sports Club Villa ambayo inakuja kucheza mechi hiyo siku ya Jumamosi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni