TIMU
ya taifa ya soka ya wanawake, Twiga Stars imewapa raha Watanzania jioni
ya leo baada ya kuifunga Malawi mabao 2-0 Uwanja wa Azam Complex,
Chamazi, Dar es Salaam katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa.
Katika mchezo huo maalum wa kumuaga mchezaji mwenzao mkongwe, aliyeitumikia timu hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja, Esther Chaburuma ‘Lunyamila’, Twiga ilipata bao moja kila kipindi.
Shukrani kwao, wafungaji wa mabao hayo, Asha Rashid Mwalala na Mwanahamisi Omar ‘Gaucho’.
Mwalala
ndiye aliyeanza kufunga dakika ya 43 kwa shuti kali akiwa mbele ya
mabeki wa Malawi baada ya kupasiwa na Gaucho aliyefunga la pili dakika
ya 82 kwa pasi ya Amina Ally.
Esther Lunyamila alicheza kwa dakika 28 kabla ya kumpisha mrithi wake wingi ya kushoto, Stumai Abdallah na alizunguka Uwanja mzima kuwaaga mashabiki kabla ya kutoka.
Twiga inayofundishwa na Rogasian Kaijage leo ilicheza vizuri na kuwapa burudani nzuri mamia ya Watanzania waliolipa kiingilio cha Sh. 1,000 kuushuhudia mchezo huo.
Kikosi cha Twiga Stars kilikuwa; Fatma Omar/Belina Julius dk58, Anastazia Anthony, Donizia Daniel, Fatuma Issa, Fatuma Bushiri, Happyness Hezron, Amina Ally, Sofia Mwasikili/Shelder Boniphace dk58, Asha Rashid ‘Mwalala’, Esther Chaburuma ‘Lunyamila’/Stumai Abdallah dk28 na Mwanahamisi Omar ‘Gaucho’ .
Malawi; Chimwembe Madise, Ruth Nyirongo, Ania Alizi, Emilly Jossam, Madina Nguluwe, Wezzie Mvula/Funny Mwale dk50, Pilirani Malola/Limbikani Chikupira dk76, Sungeni Msiska/Nkuzirile Bridget dk76, Linda Kasenda na Temwa Chawinga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni