Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limepitisha majina ya wachezaji wanne wapya wa Yanga, kipa Benno David Kakolanya, Hassan Hamisi Ramadhan ‘Kessy’, Vincent Andrew Chikupe na Juma Hassan Mahadhi kucheza Kombe la Shirikisho.
Yanga inafungua dimba na Mouloudia Olympique Bejaia Juni 19, mwaka huu, Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia, Algeria na sasa wanne hao wako huru kucheza.
Yanga ambayo imeweka kambi katika hoteli ya Rui mjini Antalya, Uturuki tangu Jumapili na itaondoka kesho kwenda Bejaia kwa ajili ya mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas Mapunda amesema kwamba wametumiwa leseni za wachezaji hao kutoka CAF.
Hassan Kessy (kushoto), Juma Mahadhi (katikati) wakiwa na Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh wakati wa safari ya Uturuki |
Kakolanya amesajiliwa kutoka Prisons ya Mbeya, wakati Kessy ametoka kwa mahasimu, Simba, Vincent ametoka Mtibwa Sugar na Mahadhi ametoka Coastal Union.
Mechi hiyo itachezeshwa na marefa wa Morocco, Bouchaib El Ahrach atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Redouane Achik na Youssef Mabrouk.
Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kuwakaribisha mabingwa wa Afrika, TP Mazembe Juni 28 katika mchezo wake wa pili wa Kundi A.
Na katika mchezo huo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limechanganya marefa kutoka nchi tatu tofauti, ambao ni Janny Sikazwe wa Zambia atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Jerson Emiliano Dos Santos wa Angola na Berhe O'michael wa Eritrea.
Timu nyingine katika Kundi A ni Medeama ya Ghana ambayo itafungua dimba na TP Mazembe mjini Lubumbashi Juni 17, mwaka huu, mchezo ambao utachezeshwa na marefa wa Shelisheli Bernard Camille, Hensley Danny Petrousse na Eldrick Adelaide.
Kikosi kamili cha Yanga kilichopo kambini Uturuki ni makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benno Kakolanya.
Mabeki; Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Pato Ngonyani, Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' na Bossou anayetarajiwa kufika leo.
Viungo; Thabani Kamusoko, Juma Mahadhi, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Godfrey Mwashiuya.
Washambuliaji; Donald Ngoma, Matheo Anthony na Amissi Tambwe.
Msafara upo chini ya Kocha Mkuu, Mholanzi, Hans van der Pluijm, Kocha Msaidizi Juma Mwambusi, Kocha wa makipa, Juma Pondamali, Daktari Edward Bavu, Mchua Misuli, Jacob Onyango, Mtunza Vifaa Mohammed Mpogolo na Meneja Hafidh Saleh.
WAKATI HUO;
Timu ya Medeama SC ya Ghana inataka kujitoa katika Kundi A michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na kukabiliwa na hali ngumu ya kifedha.
Timu hiyo inatarajiwa kuanza na waliokuwa mabingwa wa Afrika, TP Mazembe ya DRC Jumapili, siku ambayo Yanga ya Tanzania itakuwa mgeni wa MO Bejaia nchini Algeria katika mchezo mwingine wa kundi hilo.
Ofisa wa Mawasiliano wa Medeama, Benjamin Kessie amesema katika taarifa yake kwa Umoja wa Waandishi wa Habari Afrika, maarufu kama Football Africa Arena kwamba iwapo Shirikisho la Soka Afrika (CAF) halitawasaidia fedha watajitoa.
Medeama kama timu zote zilizofuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani baada ya Ligi ya Mabingwa, inapaswa kupewa dola za Kimarekani 150,000.
Hata hivyo, CAF bado haijafanya mgawo huo na timu hiyo ya Ghana ilidhani ikifuzu tu itapatiwa fedha hizo ziwasaidie kusafiri kwenda Lubumbashi, DRC kucheza na Mazembe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni