KIRAKA wa Yanga, Mnyarwanda mwenye asili ya DR Congo,
Mbuyu Twite, ndiye mchezaji aliyeweka rekodi ya kipekee kwenye kikosi hicho
mpaka sasa katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi.
Rekodi hiyo ni ile ya kucheza nafasi tatu tofauti
katika mechi tatu mfululizo za michuano hiyo ambayo Yanga imecheza mpaka sasa.
Twite ambaye kuihalisia ni kiungo mkabaji, amekuwa
akichezeshwa nafasi tofauti uwanjani na mara kadhaa huonyesha kiwango cha hali
ya juu bila ya kumuangusha kocha wake, Mholanzi, Hans van Pluijm pamoja na
benchi zima la ufundi la timu hiyo.
Kiungo huyo hivi karibuni alikuwa kwenye hatari ya
jina lake kukatwa kikosini hapo baada ya mkataba wake kumalizika, lakini mabosi
wake wakajiuliza mara mbili na kumpa mkataba mpya wa miaka miwili ambapo kwa
sasa wanaona uamuzi wao wa kumbakisha unaleta majibu chanya.
Nimemfuatilia kwa umakini mchezaji huyo katika mechi hizo
tatu na kubaini amecheza zote ambazo ni jumla ya dakika 270.
MO Bejaia vs
Yanga
Katika mchezo huu wa kwanza wa makundi uliopigwa Juni
19, mwaka huu huko nchini Algeria, ulimalizika kwa Yanga kufungwa bao 1-0.
Kwenye mchezo huu Twite alicheza beki wa kulia baada
ya Juma Abdul kuwa majeruhi huku mchezaji mpya kikosini hapo, Hassan Kessy
akizuiliwa kucheza kutokana na uhamisho wake kutoka Simba kuonekana haujakamilika.
Kwa dakika zote tisini za mchezo huo, Twite alicheza
vizuri japo siyo sana, lakini pia bao walilofungwa lilitokea upande wake ambapo
alichelewa kukaba, ikapigwa krosi iliyomkuta mfungaji, Yassin Sahli.
Yanga vs TP
Mazembe
Huu ulikuwa mchezo wa pili wa hatua hiyo. Yanga
ilikuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, mchezo huo ulimalizika kwa Yanga
kufungwa tena bao 1-0.
Kutokana na mabeki wa kushoto wa Yanga, Oscar Joshua kuwa
majeruhi huku Haji Mwinyi akitumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata walipocheza
na MO Bejaia, Twite akachukua mikoba yao na kucheza kwa dakika zote tisini.
Jumla akawa amecheza dakika 180 katika nafasi za beki wa kulia na kushoto.
Kwa kiasi kikubwa alifanikiwa kuwadhibiti
washambuliaji wa TP Mazembe ambapo baada ya kuona hapitiki kirahisi,
wakabadilisha njia ya kuipenya ngome ya Yanga.
Yanga vs Medeama
Mzunguko wa kwanza wa hatua ya makundi ukamalizika kwa
Yanga kutoka sare ya bao 1-1, mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar.
Katika mchezo huu, Pluijm akamchezesha Twite kama kiungo
mkabaji (namba sita) huku Mzimbabwe, Thabani Kamusoko akicheza kiungo wa juu
yaani mchezeshaji (namba nane).
Twite alicheza nafasi hiyo kwa dakika 78, kabla ya kupelekwa
beki ya kushoto baada ya Oscar Joshua aliyekuwa akicheza upande huo kufanyiwa
mabadiliko na kuingia Mnyarwanda, Haruna Niyonzima aliyeenda kucheza kiungo
mchezeshaji na Kamusoko kurudi kukaba chini.
Katika nafasi ya kiungo, Twite alicheza vizuri kwa
kushirikiana na Kamusoko, lakini alionekana kupungua kasi kidogo alipopelekwa
pembeni.
Katika nafasi hizo zote, imebainika kuwa licha ya
kuzimudu, lakini anacheza vizuri zaidi kiungo mkabaji huku zile zingine akisuasua
kwa namna moja ama nyingine.
mdosejr@gmail.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni