Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro hapo jana tarehe 1/9/2016, ilimpandisha tena kizimbani Katibu wa chama cha soka Manispaa ya Morogoro Kafari Maharagande anayedaiwa kutoa rushwa ya chakula chenye thamani ya shilingi za Tanzania milioni moja kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho.
Upelelezi wa shitaka la hilo umekamilika na kesi hiyo inatarajia kuanza kusikilizwa September 15 mwaka huu.
Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro ameiambia mahakama kuwa, mashahidi 12 wanatarajiwa kutoa ushahidi kuhusiana na shauri hilo ambapo vielelezo vinne vitawasilishwa katika shauri hilo.
Kafari Maragande anashtakiwa kwa tuhuma za kutoa rushwa mnamo July 24 mwaka huu katika ukumbi wa Manispaa ya Morogoro akiwa mgombea wa nafasi ya Katibu wa chama hicho kwa kuwashawishi wajumbe wa mkutano mkuu kwa kuwapa chakula chenye thamani ya shilingi milioni moja ili waweze kumchagua katika nafasi aliyokuwa akigombea.
Akisoma shitaka mbele ya hakimu mkazi wa Mkoa wa Morogoro Aizani Msaki, mwendesha mashitaka wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro amedai hatua ya mshitakiwa kutoa rushwa ya chakula kwa wajumbe wa mkutano mkuu ni kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007.
Mshitakiwa amekana shitaka hilo lenye vipengele 9 ambapo kati yake alivikubali 8 huku akikana kipengele kimoja ambacho ndicho kilichopelekea yeye kushtakiwa cha utoaji rushwa.
Mshitakiwa yupo nje kwa dhamana hadi September 15 kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni