KLABU ya Simba imetengua uteuzi wa meneja wa timu hiyo Mussa Mgosi ambapo nafasi yake imechukuliwa na Dk. Cosmas Kapinga ambaye ataanza majukumu baada ya timu kurejea kutoka kambini Afrika Kusini, Agosti 5.
Mgosi ambaye alikuwa nahodha wa kikosi cha Wekundu hao amedumu katika nafasi hiyo kwa mwaka mmoja tangu alipoteuliwa kuchukua nafasi ya Abbas Ally ambaye alibadilishiwa majukumu na kuwa mratibu wa timu hiyo.
Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mtibwa Sugar amebadilishiwa majukumu ambapo atakuwa kocha msaidizi na meneja wa timu ya vijana ya Simba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na mawasiliano ya klabu hiyo, Mgosi na Nico Nyagawa watakuwa wasaidizi wa kocha Nico Kiondo katika timu ya vijana.
Simba imefanya mageuzi makubwa ya kiutawala wakati viongozi wakuu wa klabu hiyo Rais Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Nyange ‘Kaburu’ kushikiliwa na vyombo vya dola kufuatia tuhuma za utakatishaji fedha ambapo jana ilimtambulisha Katibu mkuu wake Dk. Arnold Kashembe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni