KAMATI ya Utendaji ya Shirikishi la Soka Tanzania (TFF) imemfuta kazi kocha wa Taifa Stars, Mholanzi, Mart Nooij na habari zinasema, Kocha Msaidizi wa Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa atashika timu kwa muda, akisaidiwa na Suleiman Matola wa Simba SC.
Kamati ya Utendaji ya TFF ililazimika kufanya kikao cha dharula baada ya Stars kufungwa mabao 3-0 na Uganda jana usiku Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika mchezo wa kwanza Raundi ya kwanza kufuzu CHAN 2016.
“Katika kikao cha leo pamoja na mambo mengine ilipitia mwenendo wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) ikiwa ni pamoja na kuhudhuria mchezo kati ya Tanzania na Uganda, kama sehemu ya tathmini ya mwenendo wa timu,”imesema taarifa ya TFF usiku huu.
“Kamati ya utendaji kwa kauli moja imeamua yafuatayo: 1.Ajira ya Kocha Mkuu Maart Nooij inasitishwa mara moja kuanzia tarehe 21/June/2015. 2. Benchi lote la ufundi la Taifa stars limevunjwa kuanzia tarehe 21/06/2015. 3.Uongozi wa TFF utatangaza punde benchi jipya la ufundi la timu ya Taifa,”imemalizia taarifa hiyo fupi iluyitolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya TFF, Baraka Kizuguto.
Lakini mara baada ya mchezo huo, Nooij alisema hawezi kuondoka kwa matokeo ya uwanjani, kwa sababu ana Mkataba hadi mwaka 2016.
TFF italazimika kumlipa Nooij dola za Kimarekani zisizopungua 125, 000 (Sh. Milioni 250,000) kwa kumvunjia Mkataba, ambao ni mishahara yake ya miezi 10, kwa sababu kwa mwezi alikuwa analipwa dola 12,500 (Sh. Milioni 25).
Mabao mawili ya mshambuliaji Erisa Sekisambu na lingine la Farouk Miya yanahitimisha historia ya kocha huyo Mholanzi Tanzania.
Habari za ndani zinasema Mkwasa na kocha Msaidizi wa Simba SC, Suleiman Matola watapewa timu kwa muda- mtihani wao wa kwanza ukiwa ni kujaribu kushinda mabao 4-0 ugenini wiki mbili zijazo ili kusonga mbele CHAN.
Matokeo ya leo yamewakosesha wachezaji wa Taifa Stars donge nono la Sh. Milioni 1 kila mmoja ahadi iliyotolewa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi jan.
Mchezo wa leo unakuwa wa tano mfululizo, Taifa Stars inafungwa chini ya Nooij aliyerithi mikoba ya Mdenmark Kim Poulsen Aprili mwaka jana na kwa ujumla timu hiyo imecheza mechi tisa bila ya ushindi chini ya Mholanzi huyo.
Kwa ujumla, Nooij ameiongoza Stars katka mechi 18 tangu arithi mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen Aprili mwaka jana, kati ya hizo ameshinda tatu tu, sare sita na kufungwa tisa- akifunga mabao 17 na kufungwa 28.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni