Napenda kuchukua nafasi hii
kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi mzima wa Wizara ya afya kwa kunialika
kushirikiana nanyi katika tukio hili. Kwa namna ya pekee nikupongezeni kwa
maandalizi mazuri na kwa kuwa na wazo la kuanzisha kituo hiki ambacho
kinaongeza nguvu katika utoaji huduma za afya hapa Tanzania. Kituo hiki ni cha
kwanza katika nchi za Afrika Mashariki na kitatoa huduma za tiba,
uchunguzi na mafunzo kwa kutumia Hadubini. Ni wazi kuwa kituo hiki
kitasaidia wananchi wetu kupata huduma hapa nchini na kitawapunguzia gharama
zilizotokana na wao kwenda nje kutafuta tiba ya magonjwa haya.
Mabibi na Mabwana;
Ninafahamu kuwa ujenzi wa
Kituo hiki umewezekana kutokana na ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na
Chama cha Magonjwa ya Tumbo cha Munich. Serikali ya Tanzania imechangia
shilingi Milioni Mia Nane na Chama cha Magonjwa ya Tumbo cha Munich kupitia
msaada kutoka ELSE KRONER FRESENIUS STIFTUNG ya Ujerumani, imechangia zaidi ya
shilingi za kitanzania Bilioni Moja kwa ajili ya ununuzi wa vifaa. Huu ni
uwekezaji mkubwa sana na naomba kutumia nafasi hii kukuombeni wenzetu wa
Hospitali ya Muhimbili kuhakikisha kuwa mnakitumia kituo hiki ipasavyo huku pia
mkivitunza vifaa vilivyopo.
Mabibi na Mabwana;
Magonjwa ya mfumo wa chakula
na ini ni miongoni mwa matatizo makubwa ya kiafya yanayoikabili
dunia nzima kwa sasa. Kumbukumbu za magonjwa ya Saratani duniani zilizotolewa
mwaka 2008 zinaonyesha kuwa, jumla ya wagonjwa wapya takribani milioni tatu na
laki tano, waliugua saratani za mfumo wa chakula na ini. Kati ya hao
asilimia 65% walitoka katika nchi maskini, ikiwemo Tanzania.
Saratani ya koo la chakula na
ini, ndizo zinazoongoza katika nchi maskini ukilinganisha na nchi zilizoendelea,
zikifuatiwa na saratani ya tumbo. Hapa kwetu Tanzania, wastani wa watu 30 hadi
35 kwa kila wananchi 100,000 hufariki dunia kila mwaka kwa saratani ya koo la
chakula.
Sababu kubwa za maradhi haya
ni za mtindo wa maisha kama unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara. Pia,
magonjwa ya kuambukiza kama homa ya ini na bakteria aina ya Helikobakta, ni
sababu mojawapo ya mtu kupata saratani za mfumo wa chakula na ini.
Mabibi na Mabwana;
Ninaelewa kuwa hatuna
wataalamu wa kutosha katika huduma hii ya afya wakiwemo madaktari, wauguzi na
wataalamu wengine ili kufanikisha kuendesha kituo hiki vizuri. Mmenitaarifu
kuwa kuna Mabingwa wa Hadubini wanane (8) hapa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa
sasa, pamoja na wauguzi watano tu ambao ni wachache sana.
Katika kusaidia kukabiliana
na upungufu huu, serikali yetu itasaidia katika kufanikisha mafunzo kwa
wataalamu zaidi ndani na nje ya nchi katika maeneo haya ili walau tuwe na idadi
inayohitajika.
Nitumie nafasi hii pia
kuwaomba wenzetu wa Taasisi za Hospitali ya Taifa Muhimbili, Chuo Kikuu cha
Afya na Sayanzi za Tiba Muhimbili na Taasisi ya Saratani Ocean Road, kupanua
huduma zenu na kutoa huduma za kitaalamu zaidi kama vile upandikizaji wa figo
na nyinginezo. Pale mnapohitaji msaada kutoka serikalini, msisite kufanya hivyo
kwani suala la afya linagusa maisha ya kila mwananchi wetu.
Mabibi na Mabwana;
Pamoja na mikakati ya kutoa
huduma za tiba, nakisihi kituo hiki pamoja na taasisi wadau kufikiria namna ya
kuanzisha kinga ambayo inajumuisha chanjo kwa magonjwa kama hepatitis B na C
ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa magonjwa ya tumbo na ini (hepatology)
ikiwemo saratani ya ini. Ninaelewa kuwa katika mpango wa chanjo (Expanded
Program of Immunisation) chanjo ya Hepatitis B inatolewa kwa watoto.
Hata hivyo, jitihada
zinatakiwa kuendelea ili kujumuisha watu wazima ambao hawajapata chanjo hiyo.
Zaidi ya hayo, tafiti zinazohusu maeneo ya Afrika ni muhimu sana kwani
zitatuonesha mwelekeo na kutusaidia katika kubuni jitihada mbalimbali za
kukabiliana na matatizo ya kiafya yanayokabili nchi zetu.
Ndugu Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili;
Katika hotuba yako umetaja
upungufu mkubwa wa wafanyakazi kama moja ya changamoto. Ni kweli changamoto hii
ipo katika kila sekta, ikiwemo sekta ya afya. Hata hivyo, serikali yetu
inafanya kazi kwa bidii kukabiliana nayo ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya
wanafunzi wanaosomea shahada ya uzamili katika tiba na uuguzi.
Mabibi na Mabwana;
Sekta ya afya ni moja
ya sekta zinazoathiriwa sana na tatizo la wataalamu kuondoka kwa ajili ya
kupata maslahi bora zaidi nje ya nchi. Naelewa kuwa kwa maendeleo ya utandawazi
tuliyonayo, mtu yeyote angependa kupata maslahi bora zaidi. Serikali yetu
imekuwa ikijitahidi na inaendelea kujitahidi kuhakikisha kuwa wataalamu wetu
wanapata maslahi bora kadiri ambavyo tunamudu.
Bajeti ni ndogo, lakini
naelewa kuwa Hospitali ya Taifa ina huduma ya wagonjwa binafsi yaani
“Intramural Private Practice (IPPM)” ambayo si kwa wagonjwa binafsi tu bali pia
mifuko mbalimbali ya bima ya afya kama vile Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya (NHIF) na Mfuko wa Afya ya Jamii. Hivyo mnaweza kabisa kutumia mapato
yanayopatikana kutokana na huduma hii katika kuboresha vipato vya wataalamu
wenu. Ninaamini kuwa kama ikitumika vizuri, maslahi bora yanayosemwa hayatakuwa
popote zaidi ya hapa hapa Hospitali ya Taifa Muhimbili
Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini Muhimbili, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi za Tiba
Muhimbili na Wakurugenzi Watendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi
ya Saratani ya Ocean Road,
Kuhusiana na kudumu kwa kituo
hiki, ninafahamu kuwa marafiki zetu wa Gastroenterology Foundation of Munich na
Else Kroner Fresenius Stiftung hawataendelea kutusaidia milele. Ni wakati
muafaka sasa kwa kituo kupitia Hospitali ya Taifa Muhimbili kuwa na bajeti yake
inayojitegemea kila mwaka ambayo itajumuishwa katika bajeti yote ya mwaka bila
kutegemea bajeti ya jumla ya Hospitali.
Zaidi ya hayo, kupitia huduma
ya IPPM, kituo kifanye kazi kama kitengo kinachotengeneza mapato yaani kwa
lugha ya kigeni “business unit” ili kutengeneza mapato yake. Mapato hayo
yatumike kununua mahitaji ya kitengo kama vile vifaa tiba kuepuka kushindwa
kutoa huduma kutokana na ukosefu wa vifaa. Hii itakihakikishia kitengo kufanya
kazi vizuri muda wote na huduma zake zitakuwa endelevu.
Mabibi na Mabwana;
Nitakuwa sijatenda haki kama
sitatoa shukrani za dhati kwa “Gastroenterology Foundation of Munich” na “Else
Kronner Fresenius Stiftung” chini ya usimamizi wa Prof. Meinhard Classen kwa
jitihada zake katika kuanzishwa kwa kituo hiki na kuifanya siku ya leo kuwa ya
kukumbukwa. Ni ukweli usiopingika kuwa, ufadhili wa fedha uliofanywa na Else
Kronner- Fresenius Stiftung ambaye Mwakilishi wake Prof. Dr. H.C. Konrad Meßmer
(MESSMER) ambaye yupo hapa pamoja na kazi ya usimamizi wa mradi huu uliofanywa
na Prof. Classen binafsi kupitia Gastroenterology Foundation of Munich, haukuwa
rahisi wala nafuu.
Hawa ni watu wenye upendo wa
dhati na wenye kujali wagonjwa na zaidi wenye mapenzi na Afrika ndio wanaweza
kufanya kazi kubwa kama hii. Hivyo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania nasema
asante sana kwako Prof. Classen pamoja na rafiki zako wa Ujerumani ambao
wachache wako hapa na wale wote waliochangia katika kufanikisha kituo hiki.
Mabibi na Mabwana;
Ningependa kuchukua nafasi
hii kuishukuru Serikali ya Ujerumani kwa misaada mbalimbali iliyokwishatoa kwa
serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa watanzania. Mmekuwa pamoja
nasi mara zote siyo tu katika sekta ya afya bali pia katika sekta nyingine,
ikiwemo uongozi bora. Kama watanzania, tunathamini ushirikiano huu na tunaamini
kuwa utadumu kadiri nchi zetu mbili zitakavyodumu.
Nashukuru tena kwa
kunikaribisha hapa na sasa natamka kwamba Kituo hiki cha TIBA, UCHUNGUZI
NA MAFUNZO YA MAGONJWA NA SARATANI ZA MATUMBO NA INI CHA HOSPITALI YA TAIFA
MUHIMBILI kimezinduliwa rasmi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni