Idara ya
polisi nchini Kenya imefanya mabadiliko ya dharura katika afisi kuu za
Kaunti ya Lamu, kutokana na mashambulio yaliyosababisha vifo vya watu 60
wiki hii.
Inspekta mkuu
wa polisi nchini Kenya David Kimaiyo amechapisha katika mtandao wa
jamii Twitter, maelezo ya wakuu wa polisi katika kaunti hiyo waliofutwa
kazi mara moja, wakiwemo makamanda wa polisi.
Afisa mkuu wa kituo cha Polisi, OCS, pia amehamishwa kituo mara moja.
Hisia za wananchi
Hatua hii tayari imepokewa kwa hisia tofauti huku wakenya wengi wakielezea kutoridhishwa na adhabu hiyo.
Miongoni
mwa walioandika malalamiko yao kwa Bwana Kimaiyo, wamesema kuwa
mabadiliko yalistahili kufanyika hadi ngazi ya juu zaidi, baadhi hata
wakimtaka yeye mwenyewe kama Inspekta wa polisi kujiuzulu.
Tangu
kutokea shambulio la Jumapili usiku katika kijiji cha Mpeketoni, karibu
na kisiwa cha Lamu pwani ya Kenya, lawama zimeelekezwa kila upande, huku
baadhi wakidai kuwa wanasiasa wamehusika na wengine wakilalamikia
utepetevu wa polisi katika kutekeleza majukumu yao.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alihutubia taifa Jumanne akisisitiza kuwa ana imani kuwa mashambulio hayo yalichochewa kisiasa.
Ametoa
matamshi hayo licha ya taarifa kutoka kwa kundi la wapiganaji wa
kiislamu wa AL shabaab waliodai kuwa wao ndio waliohusika.
Acha kutukejeli - upinzani
Matamshi
ya rais Kenyatta yame kejeliwa na wanasiasa wa upinzani nchini humo
waliodai kuwa rais huyo hana ufahamu wa yale yanayoendelea nchini mwake.
Seneta
kutoka chama kikuu cha upinzani, Moses Wetangula amesema matamshi ya
rais sio ya kweli. '' Badala ya kuitisha usaidizi wa wenzetu wenye
teknolojia bora, hata tutumie ndege zisizo na rubani kuwalipua huko
waliko, tunakaa hapa Nairobi na kudai AL shabaab hawakuhusika.''
Wetangula aliambia bunge la Kenya. '' Huu ni mzaha,'' Aliongeza bwana
Wetangula.
Lakini uchunguzi uliofanywa na BBC umeonesha kuwa huenda kuna uzito kwa madai ya rais Kenyatta.
Wakaazi
wengi wa Mpeketoni waliozungumza na BBC wametueleza kuwa, wanaamini
shambulio la Jumapili usiku linatokana na mzozo wa ardhi kati ya jamii
zinazoishi huko.
Wakaazi
hao wamesema kuwa Al shabaab wamedakia tu kujigamba kwa yaliotokea huko
ila wao wanaamini kuwa ni jambo lililokuwa likitokota kwa muda mrefu.
Huku hayo
yakiarifiwa, polisi wanasemekana kuimarisha doria katika eneo la Lamu
na vitongoji vyake. Wanajeshi wachache wametumika kuimarisha usalama
hasa katika kijiji cha Mpeketoni.
Katika
taarifa zilizotufikia ni kuwa Polisi wameimarisha usalama katika mkoa wa
magharibi mwa Kenya kutokana na duru walizopokea kuwa huenda eneo hilo
likalengwa kwa shambulio.
Al
shabaab wamefanya mashambulio ya mara kwa mara katika sehemu mbali mbali
nchini Kenya tangu majeshi ya Kenya yaingie nchini Somalia mwaka wa
2011, katika oparesheni ya kuwafagia kutoka nchini humo.
Shambulio
la punde zaidi linadaiwa kufanywa kama kulipiza kisasi ya kuuawa kwa
masheikh 2 wa kiislamu katika mji wa Mombasa pwani ya Kenya hivi majuzi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni