HIVI karibuni timu ya TP Mazembe ya DR Congo ilikuwa nchini Japan kwenye
michuano ya Kombe la Dunia kwa ngazi ya klabu, lakini haikufanya vizuri baada
ya kufungwa mechi zote mbili ilizocheza.
Ndani ya kikosi cha Mazembe kulikuwa na Watanzania wawili, Mbwana Samatta
na Thomas Ulimwengu ambao walicheza mechi zote.
Licha ya timu hiyo kushindwa kufanya vizuri, lakini Samatta na Ulimwengu
wameweka rekodi ya kuwa Watanzania wa kwanza kucheza michuano hiyo mikubwa
duniani kwa ngazi ya klabu.
Mbali na rekodi hiyo, pia Ulimwengu na Samatta wameweka rekodi zingine,
ya kwanza ni ile ya kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo hakuna
Mtanzania mwingine aliyewahi kufanya hivyo, pia Samatta kuwa mfungaji bora wa
Ligi ya Mabingwa Afrika ni rekodi nyingine kwake binafsi.
Watanzania hao wote wana mafanikio kwa sasa, lakini Samatta ndiye
anaonekana kufanikiwa zaidi kuliko Ulimwengu.
Samatta ambaye alizaliwa miaka 23
iliyopita jijini Dar es Salaam, alikulia maeneo ya Mbagala, Dar na maisha yake
ya soka aliyaanzia hukohuko huku akiwa miongoni mwa mastaa wa kikosi cha timu
ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa sasa.
Siku zote wanasema ukiwa na kipaji ni nadra sana kutofanikiwa kwani
straika huyu aliweza kuichezea Mbagala Market kuanzia ligi za chini mpaka Ligi
Kuu Bara ambayo baadaye ilikuja kujulikana kwa jina la African Lyon.
Alichezea African Lyon kwa miaka miwili kuanzia mwaka 2008 mpaka 2010,
msimu wa mwaka 2010/11 akatua Simba.
Juhudi na kujitambua kwake, kukawafanya mabosi wa Mazembe kumuondoa ndani
ya kikosi cha Simba mwaka 2011 na kumpeleka DR Congo ili aichezee timu yao
ambayo yupo nayo mpaka sasa.
Ni wazi amecheza kwa mafanikio akiwa na Mazembe kiasi kwamba mara kwa
mara maskauti wanaosaka wachezaji kutoka nchi mbalimbali wamekuwa wakipiga hodi
klabuni hapo kuulizia uwezekano wa kumsajili.
Imekuwa ngumu kwa bosi wa timu hiyo, Moize Katumbi kumuachia nyota huyo,
lakini hali ilivyo kwa sasa, hana budi kukubaliana na hilo na sasa yupo kwenye
mazungumzo ya mwisho na mabosi wa KRC Genk ya Ubelgiji inayoshiriki ligi kuu
nchini humo.
Wakala wa mchezaji huyo, Jamal Kisongo, hivi karibuni alinukuliwa akisema
wapo kwenye hatua za mwisho za kumuuza Samatta kwenye timu hiyo inayoshika
nafasi ya kwanza kwenye ligi yao.
Kwa vyovyote vile, Samatta mwakani
atakuwa mchezaji wa timu hiyo ambayo wakati inaanzishwa, miaka minne mbele
Samatta ndiyo alizaliwa.
Nyota ya Samatta inazidi kung’ara
siku hadi siku baada ya hivi karibuni kutajwa kwenye orodha ya wachezaji
walioingia katika fainali ya kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wale
wanaocheza ndani ya Afrika.
Katika tuzo hiyo, Samatta anachuana na mchezaji mwenzake wa Mazembe, Mkongo,
Robert Kidiaba pamoja na Mualgeria, Boudenedjah Baghdad anayeichezea Etoile du
Sahel ya Tunisia ambapo hivi karibuni aliisaidia kutwaa ubingwa wa Kombe la
Shirikisho Afrika.
Kilichobaki ni kusubiri mpaka Januari 7, mwakani siku ambayo tuzo hizo
zinarajiwa kutolewa huko jijini Lagos, Nigeria ili kuona kama nyota yake
itang’ara tena na kujiwekea rekodi nyingine.
Samatta akijiunga na timu hiyo,
atakuwa ni mchezaji wa tatu kutoka Afrika kuwepo katika kikosi hicho msimu huu
kwani kwa sasa wapo kiungo Mghana, Bennard Kumordzi na beki Mnigeria, Onyinye
Wilfred Ndidi.
Pia kama akijiunga na timu hiyo
kabla ya Januari 17, basi anaweza kuwemo katika mchezo wa upinzani mkali wakati
timu hiyo itakapocheza na wapinzani wao wa jadi ambao kwa sasa wanashika nafasi
ya pili, Anderlecht.
Ikumbukwe K.R.C GENK kupitia akademi yao ndipo walipo tokea kina Yannick Ferreira Carrasco (Atlético Madrid), Jelle Vossen (Club Brugge), Steven Defour (RSC Anderlecht), Christian Benteke (Liverpool FC), Thibaut Courtois (Chelsea FC), Divock Origi (Liverpool FC) na Kevin De Bruyne (Manchester City FC).
Mara ya mwisho kwa klabu hii inayotumia uwanja wa Cristal Arena wenye kuchukua watazamaji 21,500 kushiriki michuano ya kombe la mabingwa barani Ulaya ilikuwa ni msimu wa 2011-12 na mara ya mwisho kushiriki michuano ya Europa Ligi ni msimu wa 2013-14.
'' PALIPO NA NIA KUNA NJIA''
IMEANDIKWA NA
OMARY SULTAN MDOSE KWA USHIRIKIANO NA MR'CHOI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni