POLISI
Mkoa wa Temeke, imewakamata vijana wawili wanaodaiwa kujifanya
waganga wanaotoa tiba kwa wanawake, ambao masharti yake ni kushiriki nao
ngono bila kinga na kuacha nguo za ndani, ili zifanyiwe dawa zaidi.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo, alidai vijana hao Juma Hemedi (32) na
Abrahman Mulsin, wote wakazi wa Tandika, baada ya kushiriki ngono na
wagonjwa wao huwaambia waache nguo za ndani.
Kamanda
Kiondo alidai baada ya kupata malalamiko, Jeshi la Polisi ilianzisha
msako na kuwapekua waganga hao, ambapo walikutwa na nguo za ndani za
kike 22, ambazo alisema zitakuwa ushahidi wa kuingiliwa kimwili kwa
wanawake hao. Vitu vingine wanavyodaiwa kukutwa navyo ni pembe, tunguli,
makopo ya dawa na vibuyu.
“Sheria
iko wazi, inasema mganga anapofanya ngono kama uganga anakuwa amebaka,
na hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu 130 sura ya 16
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002,”alisema Kamanda Kiondo.
Kwa
mujibu wa madai ya Kamanda Kiondo, vijana hao wamekuwa wakijifanya
waganga wa tiba asili, husambaza vipeperushi sehemu mbalimbali za jiji
kutafuta wateja.
Mbali
na tiba hiyo ya kupata watoto, inayotolewa kwa kushiriki ngono na
mganga, Kamanda Kiondo alidai watuhumiwa hao wamekuwa wakidai kutibu
magonjwa mengine kama kisukari, vidonda vya tumbo, nguvu za kiume,
kukuza maumbile, kupata kazi, kufaulu mtihani, mvuto wa biashara,
kumilikishwa jini na kupewa pete ya bahati.
Katika
tukio lingine, Polisi inamshikilia kijana mwingine mkazi wa Tandika
Devis Corner, Maalim Kimti Rita au kwa jina lingine, Joseph Rita
anayedaiwa kutapeli Sh milioni 11 akijidai kumfanyia dua mfanyabiashara
aweze kukuza biashara yake.
Alidai
kuna mfanyabiashara mwanamke ambaye alitoa Sh milioni 11 kwa Maalim
Rita, akidanganywa kuwa atafanyiwa uganga ili afanikiwe katika biashara
yake, lakini alipoona hakuna alichopata, akaamua kutoa taarifa Polisi.
Kamanda
Kiondo alisema jamii inapaswa kuelimishwa kuachana na mambo hayo, kwa
sababu tiba yake haipo kwa waganga wa jadi na kwamba hakuna uhusiano
kati ya kufaulu na kwenda kwa waganga isipokuwa bidii ya kazi.
“Watu
wengi wamelalamikia matukio ya namna hiyo, sasa tumeamua kuweka wazi
kwa umma kwa kuwa watu wanateketea kwa kukosa elimu… watu wanauza nyumba
magari na mali zao, kwa ajili ya kupata fedha za kupeleka kwa waganga
wakiamini kuna tiba, huu ni utapeli vijana kama hawa hawawezi kukupa
utajiri wala mtoto,” alisema Kamanda Kiondo.
Alisema
waganga hao wamepata vyeti vya kufanyia kazi hiyo ya uganga wa jadi,
lakini wanachofanya ni kinyume na kazi hiyo ambapo aliahidi vyeti vyao
kuchunguzwa, kuona wamevipataje na kuwasiliana na Wizara ya Maliasili
na Utalii, ili watambue pembe wanazotumia ni za mnyama gani.
Chanzo : Habari leo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni