Cheka (kulia) akidundana na Mthailand
Toka mwanzo wa pambano hilo tayari dalili zilionekana Cheka angeshinda kutokana na kummudu vyema mpinzani wake kwa kumsukumia makonde mazito mfululizo hali iliyomfanya Singwancha kuchoka mapema na kumwacha Cheka afanye anavyotaka kwa kumpiga kama begi la mazoezi.
Hilo lilikuwa ni pambano la kwanza kwa Cheka toka abadilishiwe adhabu ya kifungo kutoka cha ndani (gerezani) mpaka kifungo cha nje. Ilipofika raundi ya nane, Singwancha alishindwa kuendelea na pambano baada ya kupigwa vilivyo na kuamua kukubali kushindwa hivyo mwamuzi wa mchezo huo Anthon Ruta kulivunja bambano hilo na ushindi ukaenda kwa Cheka.
Baada ya pambano kumalizika Cheka alisema kuwa, amepigana pambano hilo bila kujua kama atapata pesa yake au la, lakini aliamua kupanda ulingoni kwa ajili ya kuwaridhisha mashabiki wake walijitokeza kwenye pambano hilo tofauti na angeamua kugomea.
“Namshukuru mwenyezi Mungu nimeweza kufanya vizuri kwenye pambano langu, lakini nawashukuru pia mashabiki wangu na waandishi wa habari, mnajitahidi sana kututangaza”, alisema Cheka.
“Pambano hili nimepigana kwangu mimi halina hata pesa lakini nimepigana kwa ajili ya mashabiki wangu ili waweze kuona ni kwa jinsi gani nipo fiti, salama na nauwezo wa kufanya vizuri kama watapatikana ‘masponsor’ wengine wakubwa. Angalia promoter Kaiki Siraji amejitahidi lakini hela ya kunilipa sasahivi hana”, Cheka alifafanua.
“Ningeweza kukataa kucheza lakini ningewapoteza mashabiki wangu, na mimi nawapenda mashabiki wangu. Kwa uwezo wangu na kwa juhudi zangu binafsi niliweka kambi mimi na kocha wangu kwa gharama zangu mimi mwenyewe lakini nikaja kusaidiwa kwa siku tatu ambazo nimekuwepo hapa Dar es Salaam”, aliongeza Cheka.
“Mapromota wanategemea pesa ya viiingilio vya mlangoni ili waweze kutulipa, sasa mimi nadai shilingi milioni nne, sasa hapa kunakupewa milioni nne kweli. Maana hata milioni mbili haipatikani, sasa kwangu mimi iko hivi itakuwaje kwa hawa mabondia wadogo wanaopigana kwenye mapambano ya utangulizi?”,Cheka alihoji.
Kwa upande wake Singwancha, amekubali kushindwa pambano lakini akasema kushindwa kwake kunatokana na kupata majeraha kwenye mkono wake wa kulia wakati akiwa mazoezini na kusababisha kutumia mkono wa kushoto pekee.
“Nimekubali kupoteza mchezo dhidi ya Cheka lakini hii inatokana na kuumia mkono wangu wa kulia na kunilazimu kutumia zaidi mkono wa kushoto kwa mambo yote, kujilinda na kushambulia. Unapotumia mkono mmojazaidi, unapoteza balance hivyo unatoa mwanya kwa mpinzani wako kufanya vile anavyotaka”, alisema Sengwancha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni