Jamal Kasongo ambaye ni wakala wa mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samatta anaekipiga kwenye klabu ya TP Mazembe ya Congo (DRC) amesema, tayari ameshakaa na mmiliki wa klabu hiyo Moise Katumbi kujadili juu ya kuuzwa kwa Samatta.
“Katumbi anafahamu wazi kuwa Samatta amebakiza mwaka mmoja, aliniita juzi juzi tu, kujadili suala la mtoto (Mbwana Samatta). Muda pekee kwa Katumbi kutengeneza pesa ni majira ya kiangazi mwaka huu au majira ya baridi mwezi Januari mwakani, akishindwa hapo mwezi wa nne mwakani Mbwana atakuwa mchezaji huru, ataondoka klabuni bure, Katumbi hawezi kukubali hilo”, amesema Kasongo.
“Kutokana na mazingira haya, suala la Samatta kwenda Ulaya majira ya kiangazi mwaka huu halina ubishi, lazima aondoke”, ameongeza Kasongo.
Pia Kasongo amesema Samatta alishindwa kujiunga na CSK Moscow wakati wa dirisha dogo la usajili mwezi Januari mwaka huu kutokana na kupata majeraha siku moja kabla ya kucheza mechi ya kirafiki ambayo maamuzi yangetoka moja kwa moja.
“Katika siku tatu alizofanya majaribio CSK Moscow alicheza vizuri mno, alifunga magoli matatu, siku ya kucheza mechi ya kirafiki aliumia kifundo cha mguu na hakutumika katika mchezo huo ambao ungetoa majibu. CSK wametoa muda mwingine mrefu wa majira ya kiangazi kwa Mbwana”, alimaliza Kasongo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni