Bao pekee la Ammar Jemal la dakika ya 25 kipindi cha kwanza limetosha kuisukuma nje ya mashindano timu ya Yanga kwenye mchezo wa kombe la Shirikisho barani Afrika uliomalizika jana usiku mjini Sousse, Tunisia.
Yanga waliweza kutawala mchezo kwa muda mwingi wa kipindi cha kwanza lakini hawakuweza kupata magoli kutokana na safu yao ya ushambuliaji iliyokuwa inaongozwa na Amis Tambwe na Kpah Sherman kupoteza nafasi kadhaa za kufunga.
Vijana wa Jangwani walicheza vizuri na walifanikiwa kuwabana vizuri wapinzani wao hasa kwenye eneo la katikati ambapo alicheza Salum Telela na Said Juma Makapu na kwa kiasi kikubwa waliweza kutengeneza mashambulizi kadhaa lakini washambuliaji wa Yanga hawakuwa makini kwenye umaliziaji.
Wachezaji wa Etoile du Sahel wamecheza mchezo wa kutumia nguvu nyingi huku wakijihami kwa kujilinda kwa muda mwingi wa mchezo, lakini mara kadhaa walifanya mashambulizi ya kushtukiza na kupiga mashuti ya mbali.
Kwa matokeo hayo, Yanga wameondoshwa kwenye mashindano hayo kwa wastani wa magoli 2-1 kufuatia sare ya kufungana goli 1-1 kwenye mechi ya awali iliyopigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam hivyo kuwaacha Etoile du Sahel wasonge mbele kwenye michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika kwa ngazi ya vilabu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni