Hatima ya nafasi ya pili msimu huu huenda ikajulikana wakati Simba inatarajia kuikaribisha Azam FC katika mechi ya ligi kuu Tanzania bara itakayopigwa leo jioni kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Azam wapo nafasi ya pili kwa pointi 45 baada ya kucheza mechi 23, wakati Simba wanashika nafasi ya tatu wakijikusanyia pointi 41 kufuatia kushuka dimbani mara 24.
Kama Simba wanahitaji kuchukua nafasi ya pili, wanahitaji kushinda mechi ya leo ili kufikisha pointi 44 wakisubiri mechi yao ya mwisho Mei 9 mwaka huu dhidi ya JKT Ruvu huku wakiiombea Azam itoe sare mechi moja na kufungwa mechi moja.
Baada ya mechi ya leo, Jumatano ijayo Azam wanacheza na Yanga kwenye uwanja wa Taifa na watamaliza ligi Mei 9 mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Mgambo JKT kwenye uwanja wao wa Azam Complex.
Kama Azam watafungwa na Simba halafu wakafungwa na Yanga, maana yake wataendelea kuwa na pointi 45, huku Simba wakiwa na pointi 44. Mechi ya mwisho kama Azam wakishinda dhidi ya Mgambo JKT Simba hawataweza kupata nafasi ya pili. Matokeo pekee yatakayowasaidia Simba ni kuona Azam anafungwa au kutoka sare na Mgambo baada ya kufungwa mechi mbili (mechi ya leo wanayokutana wao kwa wao na Jumatano dhidi ya Yanga).
Kama matokeo hayo yatatokea maana yake Azam itamaliza ligi ikiwa na pointi 46 ambazo Simba watazivuka kama watashinda tena mechi ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu na kufikisha ponti 47.
Hizi ni hesabu za nje ya uwanja, matokeo ya mpira wa miguu hupatikana uwanjani baada ya kumalizika kwa dakika 90 za mchezo.
Kuelekea mechi ya leo, Simba kupitia kwa afisa habari wake Hajji Manara wamesema, mechi ya leo wanaitazama kwa uzito wa hali ya juu kuhakikisha wanavuna pointi tatu.
“Kila mtu anajua umhimu wa mechi hii, tunaichukulia kwa uzito mkubwa, mechi ni kubwa, tunacheza na timu nzuri, tumejipanga kuhakikisha tunashinda. Hakuna mechi rahisi. Hata wateja wetu Yanga inakuwa mechi ngumu tukikutana lakini mwisho wa siku tunawafunga”, amesema Manara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni