Shirikisho la soka la Urusi limethibitisha kufikia
makubaliano ya kuvunja mkataba na kocha
mkuu wa timu ya Taifa ya nchi hiyo, Fabio Capello baada
ya kushindwa kutimiza malengo waliyojiwekea.
Katika taarifa yake, RFU wamemshukuru Capello kwa kazi yake aliyofanya na wamemtakia
kila la kheri katika maisha yake yajayo, huku naye akilishukuru Shirikisho hilo,
mashabiki pamoja na wachezaji kwa kutoa ushirikiano mkubwa katika kipindi chote
alichofundisha timu hiyo.
Mkataba wa Capello unatakiwa kumalizika mwaka 2018 ambapo
Urusi itahodhi kombe la Dunia, lakini maamuzi yaliyochukuliwa yanalifanya
Shirikisho hilo limlipe fidia ya paundi milioni 11.
Ripoti kutoka Urusi zinasema kwamba, kocha wa CSKA Moscow, Leonid Slutsky anapewa
nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya Capello mwenye umri wa miaka 67 ambaye amekinoa kikosi cha Urusi kwai kwa miaka mitatu.
Capello alianza kuifundisha Urusi mwaka 2012, muda mfupi
baada ya kujiuzulu kuifundisha timu ya
Taifa ya England, lakini alishindwa kuwaongoza vizuri Warusi katika fainali za
kombe la Dunia mwaka jana nchini Brazil na mwaka huu nchi hiyo imefanya vibaya
katika mechi za kufuzu kombe la Mataifa ya Ulaya 2016.
Urusi inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi G
ambapo imeshinda mechi mbili tu kati ya sita ilizocheza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni