KIUNGO Hassan Dilunga ameamua ‘kujifungia’ nyumbani kwao na kutokwenda mazoezini Yanga SC, huku uongozi wa klabu hiyo ukipanga kumchukulia hatua za kinidhamu.
Habari kutoka ndani ya Yanga SC zimesema kwamba mchezaji huyo amekuwa msumbufu tangu msimu uliopita na kwa jumla nidhamu yake imekuwa ikiwakwaza makocha.
“Tangu msimu uliopita, amekuwa anachelewa mazoezini, anachelewa kuingia kambini, hajali. Hajibidiishi kukuza kiwango chake. Yupo yupo tu,”kimesema chanzo kutoka Yanga SC.
Aidha, pamoja na timu kuanza mazoezi tangu mwezi uliopita, lakini Dilunga hajatokea kabisa licha ya kupewa taarifa hadi za kupigiwa simu na viongozi.
Haijajulikana haswa ni nini kinamsababisha Dilunga, kiungo chipukizi na mwenye kipaji kufanya afanyayo.
Na Yanga SC leo asubuhi wanaingia kambini katika hosteli za Chuo Cha Maaskofu, Kurasini mjini Dar es Salaam kujiandaa na michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Wachezaji wengine wote wa Yanga SC jana walilala katika hoteli ya Valley View, Mtaa wa Kongo, Kariakoo, Dar es Salaam na leo asubuhi wanaingia kambi hiyo ya Chuo cha Maaskofu.
Yanga SC ambayo imepangwa Kundi A pamoja na Gor Mahia ya Kenya, Telecom ya Djibout, KMKM ya Zanzibar na Khartoum-N ya Sudan, itakuwa ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini.
Mabingwa mara tano wa michuano hiyo, 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012, watafungua dimba na Gor Mahia Jumamosi jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mechi ambayo itatanguliwa na mchezo kati ya APR ya Rwanda dhidi ya Al Shandy ya Sudan Saa 8:00 mchana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni