Kiungo wa kimataifa wa Uturuki aliyesajiliwa na FC
Barcelona na kusaini mkataba wa miaka mitano na mabingwa hao wa Hispania na
Ulaya hivi karibuni, Arda Turan amepewa heshima ya kufa mtu baada ya meya wa mji wa Bayrampasa
nchini humo, Atila Aydiner kutangaza kuupa mtaa mmoja katika mji huo jina la nyota huyo.
Turan aliyezaliwa katika moja ya mitaa ya mji huo mwaka 1987,
alifanikiwa kunyakuliwa na Galatasaray mwaka 2005 kabla ya kuonekana na
Atletico Madrid ya Hispania mwaka 2011 na kuwa kipenzi cha mashabiki Vincente
Calderon.
Kusajiliwa kwake Barcelona kunamfanya awe Mturuki wa pili
kuichezea klabu hiyo baada ya golikipa Rustu Recber aliyewahi kusajiliwa na
mabingwa hao mwaka 2003 usajili uliotangazwa na kutukuzwa na vyombo vya habari
vya Uturuki.
“Tunakwenda kuuita mtaa wa jeshi, Arda Turan Street. Tayari tumekwishatuma
maamuzi yetu katika halmashauri. Arda ni fahari yetu,” alisema meya huyo katika
mapokezi ya nyota huyo nyumbani kwao Bayrampasa.
Mtaa huo uliopo Bayrampasa ndio aliokulia Arda Turan kabla
kuanza safari yake ya maisha ya soka.
Bado licha ya furaha waliokuwa nayo Waturuki kwa nyota wao
kusajiliwa Fc Barcelona kwa ada inayotarajiwa kufikia Yuro milioni 41, itawabidi
wasubiri kwa nusu msimu kabla ya kumuona nyota huyo katika nyasi za Camp Nou
kutokana na Barca kutumikia adhabu iliyotokana na FIFA kubaini kosa la timu
hiyo kuvunja sharia za usajili kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 18.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni