Mshambuliaji
Emmanuel Okwi ambaye uhamisho wake daima umekuwa ukizungukwa na maswali
kila aendako, ameingia katika utata mwingine baada ya ripoti mpya kudai
kwamba alisaini mkataba wa miaka mitano wa kuichezea timu ya
SønderjyskE licha ya timu hiyo ya Denmark kutotoa hata senti kwa klabu
yake ya Simba.
Utata
huo mpya umefuatia Wadenmark hao kutaka kumrejesha Okwi Simba kwa mkopo
wa miezi sita baada ya kukwama kuipata leseni yake ya uhamisho ya
kimataifa (ITC), ambayo Simba imesema haitaitoa hadi itakapolipwa ada ya
uhamisho dola 110,000 (sawa na Sh. milioni 220).
Kumekuwa
na mitazamo kwamba kutolewa kwa mkopo kwa Okwi Simba kunaweza kuwa ni
janja ya timu hiyo ya Denmark kuvizia Mganda huyo amalize mkataba wake
Msimbazi unaomalizika Mei mwakani ili imchukue bure.
Hata
hivyo, klabu kubwa kama ya Simba inatarajiwa kwamba ilisaini mkataba na
SønderjyskE ambao unaifunga klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Denmark kwamba
lazima ilipe deni hilo, hata kama itamleta Msimbazi kwa mkopo.
Taarifa
nyingine zinasema kuwa klabu hiyo ya Denmark imefikia uamuzi huo baada
ya kumnasa mchezaji mwenye kiwango cha juu zaidi ukilinganisha na Okwi
na gharama zake za usajili ni za chini.
Rais
wa Simba, Evans Aveva, alisema kwamba kwa sasa wao wanachofuatilia ni
kuhakikisha wanalipwa kiasi hicho cha fedha ndipo waruhusu usajili wa
njia ya mtandao ufanyike.
Aveva
aliweka wazi kwamba, walimuuza Okwi baada ya mchezaji kuangalia maslahi
yake na sasa umefika wakati klabu kuhakikisha inapata haki yake na si
kuona makosa yaliyofanyika huko nyuma yanajirudia.
Katika
uongozi wa Mwenyekiti, Ismail Aden Rage, Okwi aliuzwa kwa klabu ya
Etoile du Sahel kwa dau la Dola za Marekani 300,000 lakini fedha hizo
hazikulipwa hadi leo na baadaye mshambuliaji huyo alirejea klabu yake ya
zamani ya SC Villa na muda mfupi alijiunga na Yanga.
Mganda
huyo aliichezea Yanga katika kipindi kifupi na kurejea Simba kwa
kueleza kuwa mabingwa hao wa Tanzania Bara hawakutimiza baadhi ya
vipengele vilivyoko kwenye mkataba wake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni