Kocha wa Manchester United, Mdachi Louis Van Gaal
amethibitisha taarifa za usajili wa mlinzi wa Kiitaliano kutoka Torino, Matteo
Darmian anayetarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya tayari kuitumikia United katika
msimu ujao wa ligi na michuano mingine ya ndani na kimataifa ambayo United
inashiriki.
Darmian anakwenda kuwa mchezaji wa pili kusajiliwa
na Van Gaal katika majira haya ya joto baada ya kunaswa kwa winga wa Kidachi,
Memphis Depay na tayari Muitaliano huyo amekubali kusaini kandarasi ya miaka 4
na mashetani hao wekundu wa jiji la Manchester.
Darmian anasajiliwa United kwa ada ya uhamisho ya
pauni milioni 13 na Luis Van Gaal ameliweka wazi hilo katika mkutano maalumu na
waandishi wa habari wakati wa kumtambulisha winga raia mwenzake wa Uholanzi,
Memphis Depay.
“Nimezisoma hizo taarifa (za kusajiliwa kwa
Darmian) kwenye vyombo vya habari. Lakini ni kweli (anakuja United),”
alithibitisha Van Gaal.
Katika hatua nyingine, kocha huyo anayeelekea
kwenye msimu wake wa pili tangu avae viatu vya Mskochi David Moyes, amekataa
kupigia mstari taarifa za kuondoka kwa Mdachi mwenzake Robin Van Persie katika
klabu hiyo na kusema kuwa taarifa yoyote kuhusu hilo itatolewa na klabu ifikapo
wakati mujarrab.
“Tutakapohisi anaondoka, mtasikia kutoka
Manchester United. Hatuna hizo hisia kwa sasa,” alifafanua kocha huyo juu ya
taarifa za kusepa kwa Van Persie.
Van Gaal alikwenda mbali Zaidi na kuizungumzia
safu yake ya ushambuliaji na malengo aliyonayo juu ya maboresho yake na kusema
kuwa timu haitakurupuka kusajili mshambuliaji kwa sasa mpaka pale
itakapoonekana na timu kuwa ni muhimu.
“Tuna washambuliaji wa kutosha kwa sasa. Manchester
United haisajili tu,” alinena Van Gaal.
“Mimi sio mwalimu nnayetaka kusajili tu wachezaji
wakati wote, nataka kuendeleza wachezaji ila wakati mwingine inatubidi kusajili,”
aliongeza.
“Unaposajili ni lazima unachokisajili kiwe bora Zaidi
ya ulichonacho. Lakini hilo litaonekana msimu utakapoanza kama ni kweli
tunachokidhani juu ya wachezaji,” alisisitiza.
Luis Van gaal hakusita kuzungumzia hali ya mlinda
mlango wa United anayehusishwa na kuhamia Real Madrid, David De gea na kusifu
mwenendo wake katika kipindi chote cha maandalizi ya msimu mpya.
“Ni mchezaji wa kulipwa. Na ameonesha mwenendo
mzuri sana mpaka sasa,”
“Ni kipindi kigumu kwa kocha yoyote yule. Mchezaji
anapotaka kuondoka, wewe hutaki aondoke nab ado unatakiwa ununue wachezaji-ni
kipindi kigumu mno,” alieleza meneja huyo juu ya sakata la golikipa wake ambaye
yupo na timu akiendelea na maandalizi ya msimu mpya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni