WAKATI kiungo mkabaji Mzimbabwe, Thabani Komusoko yupo mjini Dar es Salaam kwa mipango ya kujiunga na Yanga SC, klabu hiyo inatarajiwa kupokea ugeni mwingine usiku wa leo.
Beki wa kati wa kimataifa wa Togo, Vincent Bossou anawasili usiku wa leo kwa ajili ya kujiunga na Yanga SC- na wawili hao wote kesho watafanyiwa majaribio mafupi kabla ya kufanyiwa vipimo vya afya na wakifuzu watasaini.
Bossou na Komusoko watafanya mazoezi na Yanga SC asubuhi ili makocha, Mholanzi Hans van der Pluijm na Charles Boniface Mkwawa wawaone na wakiridhika nao, watakwenda kufanyiwa vipimo vya afya, ambavyo wakifuzu pia watasaini.
Ikumbukwe dirisha la usajili kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara linafungwa kesho Saa 6:00 usiku.
Kamusoko Yanga SC ilimuona wakati ilipokutana na klabu yake, FC Platinum ya Zimbabwe katika Kombe la Shirikisho, wakati Bossou analetwa na wakala Mganda, Gibby Kalule.
Kalule ndiye aliyewauzia Yanga SC mshambuliaji Mliberia, Kpah Sean Sherman ambaye wiki iliyopita klabu hiyo imemuuza Mpumalanga Blac Aces ya Afrika Kusini.
Vincent Bossou aliyezaliwa Februari 7, mwaka 1986 mjini Kara, Togo, aliibukia klabu ya Maranatha FC ya kwao, kabla ya kusaini Etoile du Sahel ya Tunisia Januari 15, mwaka 2010 Mkataba wa miaka miwili.
Hata hivyo, Mkataba wa 'sentahafu' huyo Etoile Sportive du Sahel ulivunjwa baada ya miezi mitatu tu naye akarejea Maranatha FC Machi 18, mwaka 2010.
Mei mwaka 2011 akaenda kusaini klabu ya Navibank Saigon FC ya Vietnam, kabla ya kuhamia Becamex Binh Duong, baadaye TDC Binh Duongzote mwaka 2013, An Giang mwaka 2014 na Goyang Hi FC mwaka jana.
Alikuwepo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Togo kilichojitoa AFCON ya mwaka 2010 Angola baada ya basi la wachezaji kushambuliwa na majeshi ya waasi ikiwa njiani kuelekea kwenye fainali hizo.
Bossou, ambaye ameendelea kuwa mchezaji wa Togo hadi mwaka huu, aliwahi ‘kumvimbia’ Nahodha wa zamani wa Ivory Coast, Didier Drogba wakati wa mechi ya Kombe la Mataifa ya Afrika baina ya Ivory Coast na Togo Uwanja wa Royal Bafokeng Januari 22, 2012 mjini Rustenburg, Afrika Kusini.
Chanzo: Bin Zubeir
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni