AZAM FC imelazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo, yanaifanya kila timu ijiongezee pointi moja, Azam FC ikifikisha 26 na Simba SC ikitimiza 22 baada ya timu zote kucheza mechi 10.
Azam FC inaendelea kuwa kileleni baada ya Yanga SC nayo kulazimishwa sare ya 0-0 na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga jioni ya leo hivyo kufikisha pointi 24, wakati Simba SC ikibaki nafasi ya nne.
Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1, Azam FC wakitangulia kupitia kwa Nahodha wake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ kabla ya Simba SC kusawazisha kupitia kwa Ibrahim Salum Hajib ‘Kadabra’.
Bocco alifunga dakika ya kwanza baada ya kumzidi maarifa kipa wa Simba SC, Vincent Angban raia wa Ivory Coast kufuatia krosi ya winga Farid Mussa Malik, aliyempokonya mpira beki Mrundi, Emery Nimubona.
Azam FC iliweka kambi kwenye eneo la Simba SC kwa takriban dakika tano mfululizo baada ya bao hilo, lakini safu ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi ilihimili vishindo vyote bila kurusu mabao zaidi.
Hajib aliisawazishia Simba SC dakika ya 25 baada ya kumtoka beki Said Mourad na kumchambua vizuri kipa Aishi Manula, kufuatia pasi maridadi ya kiungo Said Ndemla.
Azam FC walionekana ‘kuchanganyikiwa’ baada ya bao hilo na kuruhusu mashambulizi zaidi ya Simba SC langoni mwao, lakini sifa zimuendee kipa Manula aliyeokoa takriban michomo miwili ya hatari, mmoja wa Danny Lyanga na mwingine wa Hajib.
Kipindi cha pili, timu zote zilirudi kwa tahadhari kuhofia kuwapa wapinzani nafasi ya kuongeza bao.
Hata hivyo, nyota ya Hajib iliendelea kung’ara uwanjani baada ya kuifungia Simba SC bao la pili dakika ya 68 kwa shuti kali baada ya kumtoka Mourad tena.
Bao hilo halikudumu sana, kwani Bocco tena aliifungia Azam FC bao la kusawazisha dakika ya 73 baada ya kuwatoka mabeki wa Simba SC.
Baada ya hapo, timu hizo zilirudi kucheza kwa kujihami zaidi licha ya mabadiliko yaliyofanywa na makocha wote, Waingereza, Stwart Hall wa Azam na Dylan Kerr wa Simba SC.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Said Mourad, Erasto Nyoni, Serge Wawa, Himid Mao/Kipre Balou dk46, Abubakar Salum/Didier Kavumbangu dk71, Jean Baptiste Mugiraneza, John Bocco, Kipre Tchetche/Mudathir Yahya dk81 na Farid Mussa.
Simba SC; Vincent Angban, Emery Nimubona/Kessy dk84, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murushid, Hassan Isihaka, Justice Majabvi, Said Ndemla, Jonas Mkude, Danny Lyanga/Kizza dk68, Ibrahim Hajib na Abdi Banda/Mwalyanzi dk81.
MATOKEO MENGINE
FT | MAJIMAJI | 1 | : | 5 | TOTO AFRICANS |
FT | MGAMBO JKT | 0 | : | 0 | YANGA |
FT | MBEYA CITY | 2 | : | 2 | MTIBWA SUGAR |
FT | KAGERA SUGAR | 1 | : | 1 | NDANDA FC |
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni