MABAO mawili ya mshambuliaji Mganda, Hamisi Friday Kiiza yametosha kuipa Simba SC ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Stand United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Kwa ushindi huo, Simba SC inapanda kileleni mwa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu, ikifikisha pointi 45, baada ya kucheza mechi 19, ikiwazidi kwa pointi mbili, mabingwa watetezi, Yanga SC ambao hata hivyo wana mchezo mmoja mkononi.
Aidha, Simba SC watalazimika kuiombea ‘dua mbaya’ Azam FC katika mchezo wake wa kesho dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga iendelee kubaki kileleni.
Azam FC itaingia kumenyana na Coastal kesho, ikiwa na pointi 42 – maana yake wakishinda kwa wastani mzuri wa mabao watarejea kileleni.
Kiiza alifunga mabao yake katika dakika za 34 na 47, hivyo sasa anaongoza kwa kufunga Ligi Kuu akifikisha mabao 16 dhidi ya 14, ya mshambuliaji wa mahasimu, Yanga SC, Mrundi Amissi Tambwe.
Stand United ilipata bao lake la kufutia machozi dakika ya 90 kupitia kwa David Ossuman. Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, African Sports imeifunga 1-0 Mgambo Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati kocha Mmalawi, Kinnah Phiri ameanza na ushindi wa 5-1 dhidi ya Toto Africans Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Ndanda FC imeifunga 1-0 Majimaji Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, wakati JKT Ruvu imelazimishwa sare ya 1-1 na Kagera Sugar Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Hassan Kessy/Mussa Mgosi dk86, Emery Nimubona, Abdi Banda, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto/Brain Majwega dk50, Jonas Mkude, Hamis Kiiza, Ibrahim Ajibu/Danny Lyanga dk66 na Said Ndemla.
Stand United: Frank Muwonge, Revocatus Richard, Seleman Mrisho, Nassor Masoud, David Ossuman, Jacob Masawe, Pastory Athanas, Amri Kiemba, Seleman Selembe/Jeremiah Katura dk49, Hassan Banda/Elias Maguli dk49 na Vitalis Mayanga/Fred Hamisi dk75.
Wakati huohuo klabu ya Simba SC, inatarajiwa kwenda Morogoro kesho kuweka kambi kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Baradhidi ya mahasimu, Yanga SC utakaofanyika Jumamosi ijayo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba itatua Moro 'Mji Kasoro Bahari' kesho ikitokea mkoani Shinyanga ambako imenyana na Stand United katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu - na hiyo ni tofauti na mazoezi ya klabu kuweka kambi Zanzibar kabla ya mchezo mahasimu wao hao.
Yanga SC ambayo ipo Mauritius ambako baada ya mchezo dhidi ya Cercle de Joachim ambapo wameibuka na ushindi watapanda ndege ya Shirika la Tanzania (ATC) kwenda kambi kisiwani Pemba.
Ikumbukwe mechi ya mzunguko wa kwanza Simba ililala 2-0, mabao ya Malimi Busungu na Amissi Tambwe.
Hata hivyo, Febaruri 20, Simba SC wataingia Uwanja wa Taifa na kocha mwingine, Mganda Jackson Mayanja aliyeichukua timu mwezi uliopita baada ya kufukuzwa Muingereza, Dylan Kerr ambaye Yanga ilimfunga 2-0 mwaka jana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni