STAY WITH US

LightBlog

Breaking

TANGAZA NASI: +255 655 442 255

TANGAZA NASI: +255 655 442 255

CHANZI OPEN SCHOOL

CHANZI OPEN SCHOOL

Ijumaa, 19 Februari 2016

KUELEKEA MCHEZO WA WATANI WA JADI, HIZI HAPA BAADHI YA REKODI ZINAZOHUSU SIMBA NA YANGA

Mechi za Simba na Yanga hazikosi kuwa na vituko, lakini vinavyojulikana zaidi ni kule ‘kukimbiana’ uwanjani ama kwa kutopeleka kabisa timu uwanjani, au kwa kugomea mchezo.
Zifuatazo ni rekodi za timu hizo kukimbiana kwenye Ligi Kuu:


05/11/1966: Mchezo ulivunjika katika dakika ya 75 baada ya Yanga kugoma kumtoa mchezaji wao Awadh Gessani aliyeamriwa atoke nje baada ya kumchezea vibaya yule wa Simba (Sunderland).
Sunderland wakapewa ushindi na baadaye kuwa bingwa wa taifa kwa mara ya pili. Kabla ya mchezo kuvunjika Yanga ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-0. Nahodha wa Yanga, Mohammed Hussein Hassan ‘Msomali’, alifungiwa na FAT kutocheza mpira kwa miezi 12 na kwamba asipewe cheo cha unahodha, na Awadh Gessani akafungiwa kutocheza mechi tatu.
Yanga ikatishia kujitoa kwenye ligi pamoja na African Sports, lakini baadaye timu hizo zikashauriwa kuendelea na ligi.


30/03/1968: Mchezo ulivunjika baada ya mchezaji wa Simba , Emmanuel Albert Mbele ‘Dubwi’, kumpiga mwamuzi Jumanne Salum katika dakika ya 20. Wakati huo Yanga ilikuwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Kitwana Manara. Mchezo huo ukapangwa kurudiwa Juni Mosi, 1968 ambapo Yanga ilishinda kwa mabao 5-0.


03/03/1969: Sunderland iligoma kabisa kutia mguu uwanjani, hivyo, FAT ikaipa Yanga ubingwa na kuitoza Sunderland faini ya shilingi 500, ambazo hata hivyo, hazikulipwa baada ya kulisuluhisha suala hilo.
18/06/1972: Sunderland iligoma kuingia uwanjani kwa kipindi cha pili kupambana na Yanga huku Yanga ikiwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Leonard Chitete. Huu ulikuwa mchezo wa marudiano wa Ligi ya Taifa, ambapo Yanga ilipewa ushindi.


10/08/1985: Simba iligomea penati iliyotolewa na mwamuzi Bakari Bendera wa Tanga katika dakika ya 84 baada ya sentahafu wake Twalib Hilal kuunawa mpira katika eneo la hatari. FAT ikaipa Yanga ushindi na kuwa bingwa wa Tanzania Bara.


26/08/1992: Yanga ilikataa kutia timu uwanjani kucheza na Simba katika mchezo wa marudiano wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara kwa kuwa tayari ilikwishatwaa ubingwa. Simba ikapewa ushindi na kisha FAT ikaipiga Yanga faini ya shilingi 250,000 ambazo zililipwa na Murtazar Dewji aliyekuwa amejiunga na timu hiyo akitokea Pan African.


25/02/1996: Simba iligoma kupeleka timu uwanjani baada ya FAT kukataa ombi lao la kuahirisha mchezo huo kwa kuwa ilikuwa inajiandaa na mechi ya Kombe la Washindi dhidi ya Chapungu FC ya Zambia, ambayo hata hivyo, haikuja kabisa. Yanga ikapewa ushindi.


KUELEKEA MCHEZO WENYEWE
JUMLA ya mechi 12 za watani wa jadi, Simba za Yanga SC za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara zimechezwa tangu mwaka 2010.
  Yanga SC wameshinda mechi nne, Simba SC wameshinda mechi tatu, wakati mechi tano zilimalizika kwa sare.
  Kitu kimoja tu Simba SC wanajivunia kwa muongo huu hadi sasa ni kuvuna mabao 15 ndani ya mechi hizo mahasimu wao waliofunga mabao 14 licha ya kuongoza kushinda idadi ya mechi.
  Ushindi wa mabao 5-0 waliopata Simba SC dhidi ya mahasimu wao hao, Mei 6, mwaka 2012 unabaki kuwa ushindi mkubwa zaidi baina ya miamba hiyo kwa muongo huu hadi sasa.
  Siku hiyo, mabao ya Simba SC yalifungwa na Emmanuel Okwi dakika ya pili na 62, Felix Sunzu kwa penalti dakika ya 56, Juma Kaseja kwa penalti dakika ya 67 na Patrick Muteesa Mafisango (sasa marehemu) kwa penalti pia dakika ya 72.
  Kipigo hicho kililipa deni la Simba SC la Juni 1, mwaka 1968 walipofungwa 5-0 pia na mahasimu wao hado, mabao ya Maulid Dilunga (sasa marehemu) dakika ya 18 kwa penalti na 43, Salehe Zimbwe dakika ya 54 na 89 na Kitwana Manara dakika ya 86.
  Lakini bado kipigo kikali zaidi kihistoria kwa mechi za watani wa jadi kinabaki kuwa cha Julai 19, mwaka 1977, Simba ilipoitandika Yanga SC 6-0, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ akifunga mabao matatu peke yake dakika za 10, 42 na 89, Jumanne Hassan 'Masimenti' mawili dakika ya 60 na 73 na Suleiman Sanga aliyejifunga dk. 20.

Mechi ya kwanza ya mahasimu muongo huu, ilichezwa Aprili 18, mwaka 2010 na Simba ikashinda 4-3, mabao yake yakifungwa na Uhuru Suleiman dakika ya tatu, Mussa Hassan Mgosi dakika ya 53 na 74 na Hillary Echesa dakika ya 90 na ushei, wakati ya watani wao yalifungwa na Athumani Iddi ‘Chuji’ dakika ya 30 na Jerry Tegete dakika ya 69 na 89. 
 
Mechi iliyofuata Oktoba 16, 2010, bao pekee la Jerson John Tegete dakika ya 70 lilitosha kuipa Yanga SC ushindi wa 1-0 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.


 Mchezo uliofuata timu hizo zilitoka sare ya 1-1 Machi 5 mwaka 2011, Yanga SC wakitangulia kupata bao kwa penalti lililofungwa na Stefano Mwasyika dakika ya 59, baada ya Juma Nyosso kumuangusha Davies Mwape, kabla ya Mussa Mgosi kuisawazishia Simba SC dakika ya73.
 
Siku hiyo, refa Orden Mbaga alizua tafrani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutokana na kwanza kwa kulikataa bao la kusawazisha la Simba, kisha akalikubali baada ya kujadiliana na msaidizi wake namba moja.

 
Mchezo uliofuata Mzambia, Davies Mwape akafunga bao pekee dakika ya 75 Oktoba 29 mwaka 2011, Yanga SC ikishinda 1-0, kabla ya Simba SC kuwashughulikia ‘kiroho mbaya’ watani wao hao katika mchezo uliofuata Mei 6 mwaka 2012 kwa kuwatandika 5-0.

 
Oktoba 3, mwaka 2013 timu hizo zilitoka sare ya 1-1, bao la Simba SC likifungwa na Amri Kiemba dakika ya tatu, kabla ya Yanag SC kusawazisha kupitia kwa Said Bahanuzi kwa penalti dakika ya 65.


Ukawadia mchezo ambao ulimfukuzisha kipa Juma Kaseja Simba SC baada ya Wekundu wa msimbazi kuchapwa 2-0 Mei 18, mwaka 2013, mabao ya Mrundi Didier Kavumbangu dakika ya tano na Mganda Hamisi Kiiza dakika ya 62.
 
Oktoba 20, mwaka 2013 Yanga SC iliongoza kwa mabao 3-0 hadi mapumziko yaliyofungwa na Mrisho Khalfan Ngassa dakika ya15 na Hamisi Kiiza dakika ya 36 na 45, kabla ya Simba SC kusawazisha yote kipindi cha pili kupitia kwa Betram Mombeki dakika ya 54, Mganda Joseph Owino dakika ya 58 na Mrundi Gilbert Kaze dakika ya 85.

 
Aprili 19, mwaka 2014 timu hizo zilitoka tena sare ya 1-1, Haroun Chanongo akitangulia kuifungia Simba SC dakika ya kabla ya Simon Msuva kuisawazishia Yanga SC dakika ya 86, wakati Oktoba 18 mwaka 2014 zilitoka 0-0.

 
Bao la Mganda Emmanuel Arnold Okwi dakika ya 52, lilitosha kuipa Simba SC ushindi wa 1-0 Machi 8, mwaka 2015 – wakati mchezo wa mwisho kuzikutanisha timu hizo, Yanga SC ilishinda 2-0 Septemba 26, mwaka 2015 mabao ya Amissi Tambwe dakika ya 44 na Malimi Busungu dakika ya 79.

 
Hiyo ilikuwa mechi ya 12 ya watani wa jadi kufanyika tangu mwaka 2010 katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC wakishinda kwa mara ya nne dhidi ya mara tatu za Simba SC. Timu hizo zinatarajiwa kukutana tena Jumamosi katika mfululizo wa Ligi Kuu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

 
Hivi unaposoma makala haya, Simba SC wapo kambini mjini Morogoro, wakati Yanga SC wapo kisiwani Pemba kwa maandalizi ya mchezo huo. Miaka miwili ya nyuma, Simba SC dhaifu ndiyo imekuwa ikikutana na Yanga SC pamoja na matokeo yote – lakini kuelekea mchezo wa Jumamnosi hali ni tofauti.


Simba SC sasa imeimarika chini ya kocha Mganda, Jackson Mayanja ikiwa inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 45 dhidi ya 43 za mahasimu, Yanga SC. Na wakizingatia wamecheza mechi moja zaidi ya Yanga, Simba SC wanajua ili kuimarisha mawindo yao ya ubingwa ambao mara ya mwisho waliutwaa mwaka 2011 ni kiasi gani wanahitaji kushinda Jumamosi.  
  
Na Yanga SC wanataka kushinda ili kurudi kileleni na kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa wao na hapo ndipo unapogundua kwamba mchezo wa Jumamosi ni mtamu zaidi kuwahi kutokea kwa muongo huu.  
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KAMATI YA TUZO IMEFANYA MCHUJO KWENYE WACHEZAJI 30 WAMEBAKI 15, MKUDE, AJIBU WAMETOLEWA, ANGALIA ORODHA

Kamati ya Tuzo za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), iliyokutana wiki hii imeteua wachezaji 15 kwa ajili ya kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa VPL msi...

TIBA YA KIIMANI

TIBA YA KIIMANI

a

a
Adbox