TAIFA
la wanamichezo limezizima baada ya kusikia taarifa za timu ya taifa ya
Chad kujiondoa katika michuano ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika
(Afcon) ambazo zitafanyika mwakani nchini Gabon.
Kama tunavyofahamu, soka letu hapa barani
Afrika limejaa changamoto nyingi sana ikiwemo ya fedha na hii inatokana na nchi
nyingi kutokuwa na uchumi mzuri kama ambavyo taifa la Chad limekuwa katika
wakati mgumu kwa hivi sasa kutokana na hali mbaya ya kifedha katika serikali
yao na kupelekea timu yao ya taifa kushindwa kusafiri kuja Tanzania kwenye
mchezo wa marejeano na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa stars.

Baada ya taarifa hiyo wanamichezo wengi wa
Tanzania wameonekana kusononeka sana kwa maana matokeo ya ushindi waliyoyapata
nchidi Chad siku chache nyuma yamefutwa ingawa pia matokeo ya Misri na Nigeria
waliyoyapata mbele ya Chad nayo yamefutwa.
Kwa hali ilivyo mpaka sasa katika Kundi G ambalo
ndiyo tukio hilo limetokea, Tanzania ni ngumu kwao kupita lakini pia ni nyepesi
kwao kupita. Tizama msimamo ulivyo mpaka sasa.
P W D L GF GA GD Pts
1. Egypt 2 1 1 0 4 1 3 4
2. Nigeria 2 0 2 0 1 1 0 2
3. Tanzania 2 0 1 1 0 3 -3 1
KWA NINI NI NGUMU;
Ngumu kwa Tanzania kwa maana sasa
watakabiliwa na michezo miwili migumu dhidi ya Misri na Nigeria michezo ambayo
itahitajika ushindi. Misri watakuja Tanzania na kisha Tanzania kwenda Nigeria.
Kwa hali ya vikosi vya timu zote, Tanzania inaonekana
kutokuwa na kikosi chenye wapambanaji wengi ukilinganisha na wapinzani wao
waliobaki.
Baada ya Chad kujitoa kumelifanya Kundi G
kuwa gumu zaidi kwa timu zote za kundi hilo kwa sababu kila timu imeathiriwa na
kujitoa kwa Chad. Misri wapo kileleni kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya
Nigeria lakini tofauti ya pointi tatu dhidi ya Tanzania.
Mchezo wa Misri dhidi ya Nigeria ni mchezo
ambao utakuwa na ushindani mkubwa sana na ni mchezo ambao utatupa matumaini Watanzania.
Endapo Nigeria ikimfunga Misri, itafikisha
pointi tano na kukaa kileleni huku Misri ikibaki na pointi zake nne na Tanzania
pointi moja, hivyo itafanya mchezo wa Stars dhidi ya Nigeria kuwa mgumu zaidi
kwa maana Nigeria ikishinda itafikisha pointi nane ambazo zitamfanya afuzu kama
kinara wa kundi, haitajalisha matokeo ya Stars na Misri, wakati huo Stars kama
nayo ikimfunga Nigeria na Misri, basi itafuzu kwa pointi saba.
Na kwa upande wa Misri, endapo ikishinda
mchezo wake dhidi ya Nigeria itamfanya kuwa na asilimia 98 za kufuzu kwa maana itafikisha
pointi saba, pointi ambazo zitamfanya Nigeria aondolewe katika kinyang’anyiro cha
kuwania kufuzu na wakati huo itatakiwa Stars imfunge Nigeria pamoja na Misri kwa
idadi kubwa ya mabao ili mwisho wa siku Stars impige gepu Misri kwa tofauti ya
mabao ya kufunga na kufungwa baada ya wote kuwa na pointi saba.
Pia kama Misri na Nigeria zikitoka sare,
itakuwa neema zaidi kwa Watanzania kwa sababu Misri itafikisha pointi tano na Nigeria
tatu, hivyo Tanzania ambayo itacheza nao wote hawa itahitajika ishinde mechi
zote hizo kwa idadi yoyote ya mabao ili afikishe pointi saba na kufuzu bial
ubishi.
Kwa maana hiyo, kimahesabu nafasi kubwa kwa
Tanzania ni kuwaombea Nigeria washinde dhidi ya Misri au walazimishe sare leo
usiku ili na sisi tujipange vyema kimapambano tuchukue pointi zote sita kwa
mataifa hayo kisha tufuzu kwa mara ya pili kwenye michuano hiyo mikubwa barani
Afrika.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni